MAFUNZO YA TUME YATAONGEZA UJUZI NA UFANISI: MKUU WA WILAYA


Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Katavi

Mkuu wa wilaya ya Mlele mkoani Katavi Bw. Majid Mwanga amesema mafunzo yaliyotolewa na Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi za Mikoa na Wilaya yatasaidia katika kuongeza ujuzi, weledi na ufanisi katika kazi ya kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama.

Mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya wilaya hiyo ameipongeza Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kutoa mafunzo hayo yaliyolenga kuwajengea uwezo wajumbe na pia kuziimarisha Kamati hizo.

”Naishukuru Tume kwa mafunzo haya nami naahidi kuwa Kamati yangu itashirikiana na Tume kwa karibu katika kutekeleza majukumu yetu ya kamati ya kusimamia Maadili ya Mahakimu wetru wa Mahakama za Mwanzo”, alisema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Bw. Onesmo Buswelu alisema wilaya ya Tanganyika itahakikisha kuwa inawalea Mahakimu wake kwa kufuata misingi ya maadili ili watekeleze jukumu lao la msingi la kutoa haki kwa kuzingatia maadili.

”Dhana ya ulezi ina nafasi kubwa kwetu kwa kuwa tunao Mahakimu wachache, na kulingana na jiografia yetu tukishindwa kuwalea vizuri watapotea na matokeo yake tutakosa huduma”, alisema Mkuu wa Wilaya.

Aidha, Bw. Buswelu alisema atatumia mikutano yake mbalimbali kuwaelimisha wananchi wa wilaya ya Tanganyika kuhusu uwepo wa Kamati za Maadili zinazopokea malalamiko ili wazifahamu na endapo watakuwa na malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa Maadili ya Maafisa Mahakama waweze kuwasilisha na kupata haki zao.

Watumishi wa Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama wamemaliza ziara ya mafunzo kwa wajumbe wa Kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya katika mikoa ya Rukwa na Katavi pamoja na wilaya zake iliyolenga 30kuwajengea uwezo na kuziimarisha kamati hizo.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Tume imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011.