MAKAMISHNA WA TUME WATEMBELEA MAHAKAMA YA TANZANIA
Mwandishi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma
Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama leo tarehe 24 Januari, 2025 wametembelea Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania lililopo jijini Dodoma na kujionea maendeleo makubwa yaliyofanywa na Mahakama katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Kamishna wa Tume na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Gerald Ndika aliwaongoza Makamishna wenzake, Wakili Bahame Tom Nyanduga na Wakili Dosca Kemilembe Mutabuzi kutembela chumba Maalum (Judiciary Visual Situation Room) ili kujionea maendelo hayo ya Tehama katika utoaji wa taarifa mbalimbali zinazoendelea katika Mahakama zote nchini.
Katika ziara hiyo kwenye Makao Makuu ya Mahakama, Makamishna hao wa Tume ya Utumishi wa Mahakama walipokelewa na Mtendaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bw. Victor Florence Kategere, ambaye aliwapeleka kwenye chumba hicho.
Wakiwa katika chumba hicho, Afisa TEHAMA Mkuu, Bi. Priscilla Joseph aliwaongoza Maafisa wenzake kutoa maelezo kuhusu ufanyaji kazi wa mifumo mbalimbali ya kurahisisha kazi za Mahakama ukiwemo Mfumo wa Usajili, Uendeshaji na Usimamizi wa Mashauri wa Kielektroniki (e-CMS) ambao umeanza kutumika tangu mwezi Novemba, 2023, Mfumo wa Kituo cha Huduma kwa Mteja(Call Center) na Mfumo wa Huduma za Dawati la Msaada(Help Desk).
Baada ya kupata maelezo hayo Makamishna hao, walionesha kufurahishwa na utendaji kazi wa mifumo hiyo kuipongeza Kurugenzi ya Teknolijia ya Habari na Mawasiliano kutokana na juhudi zake kuanzisha Chumba hicho cha kitaalamu kinachotumika katika kuzalisha, kuchambua, kuchakata, kusimamia na kutoa taarifa mbalimbali za Mahakama.