MAKAMU WA RAIS ASISITIZA UMUHIMU WA USULUHISHI KATIKA KUTATUA MIGOGORO   


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango amesisitiza umuhimu wa Mahakama ya Tanzania na wadau wake kushirikiana katika kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi na kujenga uchumi endelevu wa taifa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa wiki ya sheria leo tarehe 22 Januari, 2023 jijini Dodoma, Makamu wa Rais amesema ni lazima kuwepo kwa mfumo thabiti wa kutatua au kusuluhisha migogoro kwa kuwa njia hiyo hujenga maelewano, mapatano na ushirikiano kwa pande mbili za mgogoro baada ya shauri kumalizika.

“Usuluhishi ni njia inayoweza kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani na kuepuka gharama kubwa za kuendesha mashauri. Usuluhishi pia unaepusha visasi na watu kujichukulia sheria mkononi”, alisema.

Aidha, Dkt. Mpango alisema migogoro inayohusu masuala ya ardhi na mipaka, Pamoja na ile inayohusu mirathi inaweza kutatuliwa kwa kutumia njia ya usuluhishi na ikasaidia kurejesha amani miongozi wa wananchi.

Kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Makamu wa Rais ameipondeza Mahakama ya Tanzania kwa kuwekeza kwenye matumizi ya TEHAMA katika kurahisisha utendaji kazi. Aliongeza kuwa Tehama imeongeza ufanisi na kusogeza huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi.

“Nakupongeza pia wewe binafsi Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa kuongoza vizuri Mhimili wa Mahakama hasa katika kusimamia uboreshaji wa huduma kama vile ikiwemo matumizi ya TEHAMA, uboreshaji wa usimamizi wa mashauri, na miundominu ya majengo ya Mahakama”, alisema.

 

Alisema kauli mbiu ya Wiki ya Sheria kwa mwaka huu inakumbusha mambo mawili ya msingi mojawapo ikiwa ni matumizi ya usuluhishi kama njia ya kutatua migogoro katika jamii na umuhimu wa kuwepo kwa haki katika kujenga uchumi endelevu. Alisema kuwa ni vigumu kuwa na uchumi endelevu wakati wananchi hawana haki, hivyo aamesisitiza umuhimu wa Mahakama kuhakikisha inatoa haki kwa wakati.

Kauli mbiu ya Wiki na Siku ya Sheria kwa mwaka huu ni Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi Katika Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau.

Makamu wa Rais alisema ili kujenga imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama, Viongozi wa Mahakama hawana budi kuzifanyia kazi changamoto zilizopo ikiwemo rushwa na kuwataka kuwachukulia hatua stahiki baadhi ya watumishi wanaojihusisha na vitendo hivyo na vingine vilivyo kinyume na maadili.

Maonesho ya Wiki ya Sheria yanafanyika jijini katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma kuanzia leo na yatamalizika Januari 29, 2023. Aidha Siku ya Sheria nchini itakayofanyika tarehe 01 Februari, 2023 ambapo mgeni rasmi atakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ambayo ni Msimamizi wa shughuli za Mahakama ya Tanzania ni miongoni mwa Taasisi wadau wa utoaji haki nchini zinazoshiriki kwenye Maonesho hayo. Baadhi ya taasisi nyingine zinazoshiriki kwenye maonesho hayo ni Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Polisi, Magereza, Uhamiaji, Wizara ya Katiba na Sheria, Tume ya Kurekebisha Sheria na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.