MAMIA WAMZIKA MAMA WA KATIBU WA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama-Arusha

Mamia ya waombolezaji wakiwemo Majaji, Viongozi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na watumishi wengine wa Mahakama ni miongoni mwa mamia ya watu waliojitokeza kumzika mama mzazi wa Katibu wa Tume, marehemu Naitovuaki Mosses Lengutai aliyepumzishwa tarehe 05 Oktoba, 2024 katika makaburi ya familia yaliyopo Suye Oloirien jijini Arusha.

Ibada ya mazishi hayo ilifanyika katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (K.K.K.T) Usharika wa Moshono na kuongozwa na Baba Askofu wa KKKT Dayosisi ya Magharibi Kati- Tabora, Dkt. Kisiri Laizer na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mahakama ya Tanzania na Serikali.

Akihubiri katika ibada hiyo, Askofu Dkt. Laizer amewaasa waombolezaji wote kuishi maisha yanayompendeza Mungu, kumshukuru Mungu kwa kila jambo na kutokata tamaa hasa pale wanapokuwa katika hali ngumu za maisha ya hapa duniani.

Askofu Laizer aliyasema hayo akinukuu kitabu kitakatifu, Biblia kutoka 1Wathesalonike 5:18 unaosema ”Shukuruni kwa kila jambo, maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu” .

Akifafanua andiko hilo la Biblia, alisema kuwa Neno la Mungu linatutaka Wanadamu kumshukuru Mungu kwa kila jambo, hata kama tunapitia katika nyakati ngumu kimaisha ikiwemo msiba kwa kuwa Yesu yupo upande wetu na atatushindia magumu hayo.

Aliwakumbusha waumini kuwa, kifo kipo wakati wote hivyo, ni muhimu kila mmoja kuishi katika imani na kuwa mienendo inayompendeza Mungu ili kujiandaa na kuwa tayari wakati wote kwa kuwa hatujui siku wala saa. 

Askofu Laizer amewashauri watoto wa marehemu kuishi kwa ushirikiano na mshikamano ili kuyaendeleza yote mazuri yaliyofanywa na marehemu kwa kuwajengea ushirikiano mkubwa kati yao. 

Akitoa salamu za pole kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani aliwatia moyo wanafamilia na kuwataka kuwa wastahimilivu katika wakati huu mgumu wa majonzi ya kuondokewa na mpendwa wao.

Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Maadili na Nidhamu) Bi. Alesia Mbuya akitoa salaam za Tume kwenye msiba huo alisema marehemu amevipiga vita vilivyo vizuri, imani ameilinda hivyo tafakari inabaki kwetu kwa wanaobaki, alisema.

Viongozi wa Serikali, Mahakama na Tume waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Kiaki Nkya na Naibu Makatibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Wengine ni Naibu Wasajili, Watendaji wa Mahakama, Wakurugenzi wa Tume na Mahakama, Mahakimu na watumishi wa Tume na Mahakama ya Tanzania.Aidha mazishi hayo pia yalihudhuriwa na Mwenza wa Jaji Mkuu na Mwenza wa Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman.

Marehemu Naitovuaki Mosses Lengutai alizaliwa tarehe 15 Aprili, 1944 na kufikwa na umauti tarehe 29 Septemba, 2024. Ameacha watoto tisa (8), wajukuu 26 na vitukuu 13. Bwana ametoa na Bwana ametwaa, Jina lake lihimidiwe.