MAONESHO WIKI YA SHERIA YALETA TIJA: MSAJILI MKUU


Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya amesema kuwa maonesho ya Wiki ya Sheria ya mwaka huu  yamekuwa ya tija na kuwafikia wanachi wengi zaidi.

Akizungumza wakati akifunga Maonesho hayo yaliyofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma, Mhe. Nkya amesema utaratibu mpya wa maadhimisho ya wiki ya sheria kwa mwaka huu uliwezesha watumishi wa Mahakama pamoja na wadau kuwatembelea wananchi katika maeneo yao ya kazi na kuwapa elimu. 

“Maonesho ya mwaka huu yamekuwa na tija hasa kutokana na kutumika kwa utaratibu wa kuwafuata wananchi katika maeneo yao ya kazi, tumeweza kufikia wanachi wengi zaidi,” alisema.  

Alisema Mahakama na wadau wake walitoa elimu katika viwanja vya maonesho na pia walifanikisha kutoa kutoa elimu kwa kuwafuata wananchi kwenye maeneo ya mikusanyiko. Baadhi ya maeneo hayo ni Machinga Complex, Mnada Mpya, Sabasaba, na Stendi ya Mabasi Nanenane.

Aidha, Mahakama na wadau wake walitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule za Msingi Kilimani, Makole, Chimwanio, Kizota, Chang’ombe, Amani, Mbwanga, Kendege na Chinangali na Shule za Sekondari za Dodoma, Lukundo, Ntyuka, Nzunguni, Viwandani, Michese, Jhon Merlin, Al Qaem Seminary, na Shule ya Wasichana Huruma, ambapo wanafunzi hao walipata fursa ya kujifunza kuhusu Mahakama pamoja na huduma zinazotolewa na Mahakama.

Msajili Mkuu aliwashukuru wadau pamoja na wananchi kwa kushirikiana na Mahakama katika kufanikisha Maonesho ya Wiki ya Sheria.

Naye Msajili wa Mahakama ya Rufani na Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya Wiki ya Sheria, Mhe. Charles Magesa akitoa taarifa ya Maonesho hayo alisema jumla ya wananchi 3,394 walitembelea Maonesho hayo.

“Kwa upande wa elimu mashuleni, jumla ya wanafunzi na walimu 13,979 walipatiwa  elimu ya sheria. Shule zilizopatiwa elimu hiyo mkoani Dodoma ni pamoja shule ya msingi ya Kilimani, Makole, Chamwino, Kizota, Chang’ombe, Amani, Kiwanja cha Ndege, Mbwanga, Mlimwa na Chinangali.” alisema Mhe. Magesa.

Katika Maonesho hayo, jumla ya Taasisi wadau 39 zilishiriki pamoja na Mahakama ya Tanzania. Baadhi ya Taasisi hizo ni pamoja na Tume ya Utumishi ya Mahakama, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Taasisi nyingine ni Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Tume ya Kurekebisha Sheria, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu Wa Serikali, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi,  Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  na Wizara ya Katiba na Sheria.