MCHANGO WA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA KATIKA USIMAMIZI WA MAADILI
MCHANGO WA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA KATIKA USIMAMIZI WA MAADILI
Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Tume imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011.
Kwa mujibu wa Muundo wa Tume, Mwenyekiti ni Jaji Mkuu, na wajumbe ni Jaji mmoja anayeteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa Majaji wa Rufani, Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa nafasi yake, Jaji Kiongozi kwa nafasi yake; na Wanasheria wawili wa kujitegemea ambao wanateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, Tume ya Utumishi wa Mahakama inayo Sekretariet ambayo ndiyo mtekelezaji wa shughuli za kila siku za Tume. Sekretariet ya Tume inayo wataalamu wa kada mbalimbali (vitengo 10) na inaongozwa na Katibu wa Tume ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama. Sekretariet hii inao Naibu makatibu wawili wanaoshughulikia masuala ya ajira na nidhamu.
Naibu Katibu wa Tume (Nidhamu na Maadili) bibi Alesia Alex Mbuya alisema majukumu ya Tume yameainishwa na Ibara 113(1) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Kifungu Na. 29 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011. Majukumu hayo ni pamoja na kumshauri Rais kuhusu uteuzi wa Jaji Kiongozi na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Msajili Mkuu, Msajili wa Mahakama ya Rufani na Msajili wa Mahakama Kuu
Tume pia inamshauri Rais kuhusu kutokuwa na uwezo kwa Jaji wa Rufani, Jaji Kiongozi au Jaji wa Mahakama Kuu kutekeleza majukumu ya ofisi, mwenendo usioridhisha wa Jaji wa Rufani, Jaji Kiongozi, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Msajili Mkuu, Msajili wa Mahakama ya Rufani na Msajili wa Mahakama Kuu, Maslahi ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania.
Jukumu lingine la Tume ni kuchambua malalamiko dhidi ya Jaji wa Rufani, Jaji Kiongozi, au Afisa yeyote wa Mahakama, na kuchukua hatua za kiutawala dhidi ya Jaji wa Rufani, Jaji Kiongozi, au Jaji mbali na hatua zilizoainishwa katika Katiba.
Tume pia inalo jukumu la kuteua, kupandisha cheo na kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya Maafisa wa Mahakama, kuajiri na kupandisha cheo au kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya mtumishi yeyote ambaye siyo afisa Mahakama kama ilivyoainishwa katika sheria.
Kutokana na ukubwa wa Mahakama ya Tanzania, Tume katika kutekeleza jukumu lake la kusimamia nidhamu na maadili ya Maafisa Mahakama imekasimu majukumu yake kwa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi za mikoa na wilaya.
Alisema kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama za Mikoa na Wilaya zinaundwa chini ya kifungu cha 50 cha sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na 4 ya 2011 ambapo wajumbe wake ni Mkuu wa Mkoa ambaye ni Mwenyekiti, Hakimu Mfawidhi wa Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa ambaye atakuwa Katibu (katika mikoa ambayo haina ofisi ya Mwanasheria wa Serikali) na wajumbe wengine wawili, watakaoteuliwa na Mkuu wa Mkoa, Maafisa Mahakama wawili watakaoteuliwa na Jaji Mfawidhi, na Mwanasheria wa Serikali Mfawidhi katika mikoa yenye ofisi ya Mwanasherika Mkuu wa Serikali, atakuwa Katibu wa kamati hiyo.
Alisema katika ngazi ya wilaya, kamati inaundwa chini ya kifungu cha 51 cha sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na 4 ya 2011 ambapo wajumbe wake ni Mkuu wa Wilaya ambaye atakuwa Mwenyekiti, Hakimu Mfawidhi wa Wilaya, Katibu Tawala wa Wilaya ambaye atakuwa Katibu, wajumbe wengine wawili, watakaoteuliwa na Mkuu wa Wilaya na Mahakimu wawili watakaoteuliwa na Jaji Mfawidhi.
Akizungumzia majukumu ya kamati za mikoa na wilaya, Naibu Katibu huyo alisema Kamati za Maadili za Maafisa Mahakama ngazi za Mikoa na Wilaya zinayo majukumu ya kupokea na kuchunguza malalamiko aliyowasilishwa dhidi ya Mahakimu Mkoa/Wilaya husika na kisha kuwasilisha taarifa kwenye Tume.
Alisema jukumu lingine la kamati hizo ni kufanya uchunguzi wa mwenendo wa Hakimu kwa kuzingatia maelekezo ya Jaji Mfawidhi na kuripoti kwake au kuchukua hatua muafaka kulingana na sheria.
Aidha, Bibi Mbuya alifafanua kuwa Kamati ya Mkoa hushughulikia nidhamu kwa Mahakimu wa Wilaya, na Kamati ya Wilaya hushughulikia nidhamu kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo.
Kwa upande wake, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kamati za maadili ngazi za mikoa na wilaya zinazoongozwa na wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya zinaisaidia Tume katika kusimamia nidhamu na Maadili ya Mahakimu kwenye mikoa na wilaya husika. Alitoa wito kwa wananchi wote wenye malalamiko yanayohusu nidhamu na maadili kuwasilisha malalamiko yao kwenye kamati hizo.
Akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria katika mafunzo kwa kamati hiyo yaliyoandaliwa na Tume kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu muundo na majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama zikiwemo Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi za mikoa na wilaya, Prof. Ole Gabriel alisema uwepo wa Kamati hizo za Maadili utasaidia kusimamia nidhamu na Maadili ya Watumishi wa Mahakama na hivyo kuboresha utendaji wa Maafisa wa Mahakama katika ngazi zote.
“Nitumie nafasi hii kuwaomba wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kutusaidia kuwaelimisha wananchi kuhusu uwepo wa Kamati hizi ili waweze kuleta malalamiko yao dhidi ya ukiukwaji wa maadili”, alisema.
Malalamiko yatakayowasilishwa kwenye kamati za maadili ni yale yanayohusu ukiukaji wa maadili pekee kwa Maafisa wa Mahakama. Kwa mujibu wa kifungu cha 41(1) cha sheria ya Usimamizi wa Mahakama, malalamiko yote yanapaswa kuwasilishwa kwa maandishi ambapo mlalamikaji anapaswa kuonesha jina lake, sahihi yake, anuani ya posta au makazi na namba ya simu ya mkononi. Kukosekana kwa kimojawapo hakuondolei malalamiko sifa.
Katika kufanikisha na kuboresha mchango unaotolewa na Wenyeviti wa Kamati za Maadili ngazi ya mikoa na wilaya, Katibu wa Tume alisema hivi sasa Tume inaziimarisha kamati hizo kwa kuzijengea uwezo, kuitangaza Tume, pamoja na kamati za maadili zake za maadili ili wananchi waweze kuzitumia.
Prof. Ole Gabriel alisema ili wananchi waweze kufaidika na huduma zitolewazo na Mahakama katika kutoa haki, hawana budi kuelewa kazi za Tume ya Utumishi wa Mahakama, na zile za Kamati zake na umuhimu wa Tume katika kusimamia utendaji kazi wa Mhimili huo.
Alisema Tume imefanikiwa katika kutekeleza jukumu lake la msingi kwa kuwa nidhamu na Maadili ya Watumishi wa Mahakama yanasimamiwa kikamilifu kupitia Kamati za Maadili za Ngazi zote na hivyo kuboresha utendaji wa Maafisa wa Mahakama katika ngazi zote.