MENEJIMENTI TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA YAKAGUA UJENZI WA JENGO LA TUME DODOMA


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama-Dodoma

Wajumbe wa kikao cha Menejimenti ya Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama wametembelea na kukagua ujenzi wa jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama unaoendelea jijini Dodoma.

Wajumbe hao walijionea maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo la ofisi za Tume linalojengwa kwenye kiwanja namba 3 Block D katika eneo la NCC, pembeni ya jengo la makao makuu ya Mahakama ya Tanzania. Ujenzi huo hivi sasa uko katika hatua ya kuweka zege kwenye msingi kabla ya kuweka nondo (Blanding stage).

Aidha kiwanja kinachotumika kujenga jengo hilo kina ukubwa wa mita za mraba 9,590, na kina hati yenye namba DOM008194 iliyotolewa tarehe 22 Julai, 2022.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Ugavi cha Tume ya Utumishi wa Mahakama, Jengo hilo linatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi Bilioni 14.3 (14,300,000,000) na Mzabuni wa jengo hilo ni CRJE (EAST AFRICA) LTD.

Mkataba wa ujenzi ulisainiwa tarehe 7 Oktoba 2022 na Mkandarasi alikabidhiwa site tarehe 10 Oktoba, 2022. Jengo hilo linatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni mwaka 2023.  

Tume ya Utumishi wa Mahakama imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011. Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania.