MKOA WA KAGERA WARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA MAHAKAMA


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama- Kagera

Mkuu wa Mkoa wa Kagera ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa Mhe. Fatma Mwassa amesema mkoa wa Kagera unaridhishwa na utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania.

Akizungumza na Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma mara baada ya kumpokea katika kiwanja cha Ndege cha mjini Bukoba, Mkuu huyo wa Mkoa alisema wana Kagera wanaridhishwa na Utendaji kazi wa Mahakama na kasi ya kushughulikia migogoro na mashauri ni kubwa.

”Sisi wana Kagera pamoja na kuwa tuna kesi nyingi zile ngumu lakina tunaridhishwa sana na utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania”, alisema Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Alisema mkoa wa Kagera umeanza jitihada za kupunguza migogoro ile ambayo si lazima ifike mahakamani. Aliongeza kuwa wamejipanga kutoa mafunzo maalum kwa Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na viongozi wengine ili kuwajengea uwezo wa namna ya kushughulikia migogoro midogo midogo ambayo haina ulazima wa kufikishwa mahakamani. Mafunzo hayo yatatolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba.

Akielezea hali ya mauaji katika mkoa wa Kagera, Mhe. Mwassa alisema hivi sasa mkoa wake unaendesha kampeni kubwa ya kudhibiti mauaji na kwamba vitendo hivyo vimepungua na kwa mujibu wa ripoti ya Polisi, mkoa huo umetoka kuwa mkoa unaoongoza kwa kuwa na kesi nyingi za mauaji.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania alisema Makamishna wa Tume wamewasili mkoani Kagera kuanza ziara katika mikoa ya Kagera na Geita yenye  lengo la kukutana na Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuimarisha utendaji kazi wa kamati hizo ikiwa ni panoja na kuangalia maeneo yanayohitaji mabadiliko ya kanuni.

”Tume iko Dar es salaam lakini shughuli nyingi za usimamizi wa maadili ya Maafisa Mahakama zinafanyika nchini kote, viongozi wa mikoa na wilaya ni wawakilishi wa Tume”, alisema Jaji Mkuu.

Alisema katika ziara ya Tume kwenye mikoa ya Kagera na Geita, Makamishna wa Tume pia watapata nafasi ya kukutana na Watumishi wa Mahakama pamoja na viongozi na kuangalia maeneo yanayohitaji miundiombinu ya Mahakama ili kuboresha huduma za utoaji haki.

Tume ya Utumishi wa Mahakama inatarajiwa kuanzia ziara ya siku nne katika mikoa ya Kagera na Geita yenye lengo la kuimarisha utendaji kazi wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama. Ziara hiyo itaanza kesho tarehe 9 Oktoba na kumalizika tarehe 12 Oktoba, 2023.