MKUU WA MKOA WA KATAVI AISHAURI TUME KUWAELIMISHA WANANCHI UWEPO WA KAMATI ZA MAADILI


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama-Katavi

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko ameishauri Tume ya Utumishi wa Mahakama kuendelea na jitihada zake za kuwaelimisha wananchi kuhusu uwepo wa kamati za maadili ya Maafisa Mahakama na namna ya kuwasilisha kwa wakati malalamiko yao yanayohusu ukiukwaji wa maadili ya Maafisa hao.

Akizungumza na watumishi wa Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama jana mkoani humo, Mkuu huyo wa Mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya Mkoa alisema wapo wanannchi wanaoweza kuwa na malalamiko lakini hawajui ni wapi wayapeleke.

”Waelimisheni wananchi ili waweze kuwasilisha kwa wakati malalamiko yao ndani ya muda wa miezi sita         uliowekwa na Kanuni za Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya ili wapate haki zao”, alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alisema mafunzo waliyopatiwa na Tume kuhusu namna ya uendeshaji wa kamati hizo yatawasaidia kujinoa zaidi na kujiweka sawa pindi watakapopokea malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa Maadili ya Maafisa Mahakama na kuyashughulikia kwa kufuata utaratibu, Kanuni na miongozo iliyowekwa na Tume.  

”Sasa tumepata mwanga, tutakapokuwa tunaendelea kuzipitia kanuni na mwongozo wa uendeshaji wa kamati hizo, tutaweza kutekeleza vema jukumu hili muhimu la kisheria”, alisema.

Alisema Ofisi yake itaendeleza ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na Mahakama ya Tanzania na pia aliipongeza Tume kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo kwa wajumbe wa Kamati za Maadili hususan Wenyeviti na Makatibu wa Kamati hizo.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Mpanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya wilaya Bi. Jamila Kimaro aliishauri Tume kuzijengea uwezo kamati hizo ili ziweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Alisema Ofisi yake imekuwa ikitekeleza vema takwa la kisheria la kuitisha vikao vya kamati mara nne kwa mwaka kama inavyopaswa na pia kutenga fedha kwa ajili ya kuendesha kamati hizo.   

Naye Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Nidhamu na Maadili) Bi. Alesia Mbuya ameishauri Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya wilaya ya Mpanda kusimamia nidhamu na maadili ya Mahakimu na kufanya jukumu la ulezi wa Maafisa hao wanapotekeleza majukumu yao.

Aliwataka Mahakimu kuwa na weledi katika kazi yao na kuzingatia nidhamu na maadili wanapotekeleza jukumu lao la msingi na la kikatiba walilopewa la kutoa haki kwa wananchi.

Watumishi wa Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaendelea na kazi ya utoaji wa mafunzo kwa wajumbe wa Kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya katika mikoa ya Rukwa na Katavi pamoja na wilaya zake kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuziimarisha kamati hizo.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Tume imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011.