TUME YAMUAGA PROF. JUMA NA KUMKARIBISHA MWENYEKITI MPYA
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma
Tume ya Utumishi wa Mahakama, imemuaga rasmi aliyekuwa Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma na kumkaribisha Mwenyekiti mpya, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Mcheche Masaju.
Katika kikao chake maalum kilichofanyika jana tarehe 11 Julai, 2025 kwenye ofisi za Tume jijini Dodoma, Makamishna wa Tume wakiongozwa na Mwenyekiti wao Mhe. Masaju walimpongeza Prof. Juma kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa Tume na Mahakama ya Tanzania hususan maboresho ya huduma za Mahakama.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania alimshukuru na kumpongeza Mwenyekiti Mstaafu wa Tume kwa utumishi uliotukuka pamoja na kumuelezea kuwa ni mtu mkarimu, mbunifu na mwepesi wa kushirikisha wengine utaalamu alionao kwa lengo la kuhakikisha nao wanafanikiwa katika utendaji kazi wao.
Aidha, Makamishna wa Tume walimpongeza Jaji Mkuu kwa kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na kuahidi kumpa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha kuwa Tume inaendelea kutekeleza ipasavyo wajibu wake na kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa chini ya Uongozi uliopita.
Makamishna hao wa Tume, kwa nyakati tofauti walimpongeza Mwenyekiti aliyemaliza muda wake kwa kazi kubwa aliyoifanya ya uboreshaji wa huduma za kimahakama hususan ujenzi wa majengo ya kisasa ya Mahakama, kuanzisha mifumo mbalimbali ya Tehama na kupunguza au kuondoa matumizi ya mbinu za kiufundi katika utoaji haki.
Walisema katika kipindi chake, kumekuwa na mabadiliko kadhaa ya sheria na kanuni zinazohusika na utoaji wa haki na kupanuka kwa Mahakama ya Rufani pamoja na Mahakama Kuu ya Tanzania kupitia ongezeko la idadi ya Majaji. Wakitolea mfano wa Mahakama ya Rufani walisema kulikuwa na Majaji 16 wakati akiteuliwa kuwa Jaji Mkuu na Mwenyekiti wa Tume na sasa idadi ya Majaji hao imeongezeka na kufikia 37.
Kuhusu kuboreshwa kwa maslahi ya watumishi wa Mahakama, Makamishna hao walimpongeza Prof. Juma kwa juhudi zake katika kutetea maslahi ya watumishi ambapo maslahi ya Majaji na Mahakimu yameboreshwa na bado juhudi zinaendelezwa kwa watumishi wa kada nyingine.
Kwa upande wake Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania na aliyekuwa na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis amewaasa Makamishna wa Tume kuwa wabunifu zaidi ili Tume na Mahakama ya Tanzania isonge mbele.
”Siku zote Taasisi ni lazima iwe na ubunifu, ukibaki na Sheria zilezile na mifumo ile ile hauwezi kufanikiwa kwa kuwa jamii inabadilika kwa kasi sana”, alisema Prof. Juma.
Aliwataka kufikiria mabadiliko siku zote ili Tume ya Utumishi wa Mahakama na Mahakama ya Tanzania iweze kuendelea zaidi na zaidi. Aidha aliwaasa Makamishna hao wa Tume kushirikiana na kumpa ushirikiano wa karibu Mwenyekiti Mpya wa Tume kwa kuwa safari ya maboresho ya huduma za Mahakama mtu mmoja hawezi kufanya peke yake.