MSAJILI MKUU MAHAKAMA ATOA WITO WANANCHI KUTEMBELEA MAONESHO WIKI YA SHERIA


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama-Dodoma

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma ametoa wito kwa wakazi wa Dodoma na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kutembelea maonesho ya wiki ya Sheria yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square ili kupata uelewa wa masuala mbalimbali ya kisheria.

Akizungumza na Waandishi wa habari viwanjani hapo mara baada ya kutembelea mabanda mbalimbali ya wadau wa Mahakama, Msajili Mkuu alisema Maonesho hayo yana umuhimu mkubwa kwa kuwa yanatoa uelewa mkubwa wa masuala yanayohusu sekta ya sheria.

Alisema wananchi watakapotembelea maonesho hayo watakutana na wataalamu mbalimbali wa masuala ya sheria wa Mahakama pamoja na wadau wake na kujifunza mengi kuhusu sekta ya sheria kwa ujumla.

Akizungumzia kauli mbiu ya wiki ya Sheria kwa mwaka huu, Msajili Mkuu alisema wananchi hawana budi kuielewa dhana iliyopo kwenye Kauli mbiu hiyo ili waweze kutumia muda mwingi katika kufanya shughuli za uzalishaji maji. Kauli mbiu ya mwaka huu ni Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi Katika Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau.

“Faida za matumizi ya usuluhishi kama njia ya kutatua migogoro katika jamii ni Pamoja na kuleta utengamano, kuepusha chuki na husuda miongoni mwa watu, kuokoa muda na gharama zitakazotumika kuendesha shauri mahakamani.

Kuhusu Maonesho ya wiki ya Sheria ya mwaka huu, Mhe. Chuma ameyaelezea kuwa yana mwamko mkubwa zaidi kwa wananchi na pia taasisi za wadau zilizoshiriki. Aliongeza kuwa mwaka huu idadi ya Taasisi zilizoshiriki imeongezeka.

Maonesho ya wiki ya Sheria yanafanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma. Maonesho hayo yalizinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango tarehe 22 Januari, 2023 na yatamalizika Januari 29, 2023.