MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AAPISHWA KUWA KAMISHNA WA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim, Hamis Juma leo tarehe 7 Septemba, 2024 amemuapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari kuwa Kamishna wa Tume hiyo.

Mhe. Johari ameapishwa kuwa Kamishna wa Tume kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na. 4 Sura ya 237 kinachomtaka kila Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kuapishwa na Mwenyekiti wa Tume kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yake. Anachukua nafasi hiyo baada ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa hivi karibuni.

Akizungumza baada ya kumuapisha Kamishna huyo, Jaji Mkuu wa Tanzania alimtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa ushirikiano kwa Mahakama ya Tanzania pamoja na taasisi nyingine na pia kushiriki kwenye vikao mbalimbali vya Tume ya Utumishi wa Mahakama.

“Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kiungo muhimu katika kuunganisha Mihimili ya nchi, hivyo sisi kwa upande wetu wa Mahakama tunamtegemea sana katika kututetea na kutusemea kwenye masuala mbalimbali yanayohusu Mahakama, alisema”.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu alimshukuru aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Dkt. Feleshi kwa kazi kubwa aliyofanya na kwa mchango aliotoa alipokuwa Kamishna wa Tume kwa kipindi cha miaka sita.

”Umekuwa daraja muhimu sana ambapo umetuunganisha sisi na mihimili mingine, lakini pia ulishiriki vikao na ziara za Tume licha ya majukumu mengine makubwa uliyokuwa nayo, tunakushukuru sana”, alisema Jaji Mkuu.

Akizungumza mara baada ya kuapishwa kuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameahidi kutoa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Tume.

“Napenda kuchukua fursa hii kuwaahidi kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu itachukua nafasi yake stahiki na kutoa mchango wake ipasavyo katika katika shughuli za Tume na kuhakikisha kwamba tunakuwa daraja zuri kwa Mihimili ya nchi katika kutekeleza majukumu yake” alisema.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna ya Tume ya Utumishi wa Mahakama aliyemaliza muda wake Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Dkt Eliezer Mbuki Feleshi amemuasa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendeleza ushirikiano na Tume na kuisaidia inatekeleza majukumu yake.

Kwa mujibu wa Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Utumishi wa Mahakama inaundwa na wajumbe wafuatao; Jaji Mkuu ambaye ni Mwenyekiti, wajumbe wengine wa Tume ni Mwanasheria Mkuu wa Serikal, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji mmoja wa Mahakama ya Rufani ambaye anateuliwa na Rais, pamoja na wajumbe wawili wanaoteuliwa na Rais. Aidha, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ni Katibu wa Tume na ndiye mtekelezaji wa maamuzi yote ya Tume.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania