MWENYEKITI KAMATI YA MAADILI WILAYA AIPONGEZA MAHAKAMA


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama,Dodoma

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama mkoani humo, Alhaji Jabir Mussa Shekimweri ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa uboreshaji wa huduma zake pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya Sheria.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa pongezi hizo leo tarehe 31 Januari, 2025 alipotembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika katika Viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

“Naushukuru na kuupongeza sana Mhimili wa Mahakama ya Tanzania kwa maboresho na kwa kuendelea kuadhimisha wiki na siku ya sheria, na kuendelea kufanya maonesho haya kitaifa Dodoma,” alisema Alhaji Shekimweri.

Akizungumzia Kaulimbiu ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria ya mwaka huu “Tanzania ya 2050: Nafasi Ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika kufikia malengo makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo,”, Mkuu wa Wilaya huyo alisema kazi ya Mahakama ni muhimu katika kuinua Taifa.

Amesema kuwa, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama huku akitoa rai kwa wananchi kutembelea maonesho ya Wiki ya Sheria ili waweze kupata fursa ya kupatiwa elimu ya Mahakama na masuala mengine yanayohusu Sheria kwa ujumla.

Maonesho ya Wiki ya Sheria yatamalizika kesho Jumamosi tarehe 01 Februari, 2025 ambapo kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini yatafanyika tarehe 3, Februari, 2025 katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma na Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.