NAIBU KATIBU ATOA RAI WAJUMBE KAMATI ZA MAADILI KUWA WAADILIFU


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Shinyanga

Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Maadili na Nidhamu) Bi. Alesia Mbuya amesema ili jukumu la msingi la kutoa haki litimizwe na wale wote waliopewa jukumu la kusimamia haki, suala la kuzingatia maadili ni la lazima na muhimu kwao.

Akizungumza wakati wa Mafunzo ya siku mbili kwa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa na wilaya yaliyoanza leo mkoani Shinyanga Naibu Katibu alisema kuwa Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeipa Mahakama ya Tanzania jukumu la msingi la kutoa haki bila upendeleo na kwa wakati.

Alisema Ibara ya 113 (1) ya Katiba ikisomwa pamoja na kifungu Na. 29 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama sura ya 237 ndiyo inayoipa Tume mamlaka ya kusimamia maadili ya Mahakimu wanaohudumu katika Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi. Aliongeza kuwa jukumu hili pia limekasimiwa kwenye Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi za Mikoa na Wilaya.

Alifafanua kuwa ili kuimarisha uwazi na uwakilishi, muundo wa Kamati hizo umejumuisha makundi mbalimbali ya kijamii na Kiserikali ikiwemo Viongozi wa Serikali, Mahakimu, Viongozi wa dini na Wawakilishi wa wananchi ili kuhakikisha kuwa uamuzi unaotolewa na Kamati unakuwa wa haki na wenye kuzingatia maslahi ya pande zote mbili.

Akielezea sababu za kufanyika kwa Mafunzo hayo, Naibu Katibu alisema Tume imeona kuna umuhimu wa kuandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati za Maadili ili waweze kufanya kazi kwa weledi na kwa ufanisi.

”Hii ni fursa ya pekee ya kubadilishana uzoefu, kuongeza uelewa na kupata majibu ya changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya Kamati”, alisisitiza Naibu Katibu.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama kutoka wilaya ya Kahama Mchungaji wa Kanisa la Ephata, Novatus Robert aliishauri Sekretarieti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kuongeza kasi ya utoaji wa elimu kwa wananchi kwa njia mbalimbali na kwa lugha nyepesi ili wananchi wengi zaidi wafahamu kuhusu uwepo wa kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama na kuzitumia kamati hizo katika kuwasilisha malalamiko yao yanayohusu ukiukwaji wa maadili ya Mahakimu.

Katika mafunzo hayo baadhi ya wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama waliapishwa ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na Mwenyekiti Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama mkoani humo Mhe. Mboni Mhita, Katibu Tawala wa Wilaya  pamoja na Wenyeviti wa Kamati za Maadili wa wilaya za Kishapu, Kahama na Shinyanga.