NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA ATEMBELEA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Abdalah Sagini leo tarehe 23 Septemba, 2024 ametembelea Ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama jijini Dar es salaam na kuzungumza na Watumishi wa Sekretariet ya Tume hiyo.

Ziara ya Naibu Waziri huyo ni ya kwanza katika ofisi hizo za Tume tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri wa wizara hiyo hivi karibuni.

Katika ziara hiyo ya kikazi, Naibu Waziri Sagini alipokewa na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel ambapo pamoja na mambo mengine alipata wasaa wa kuzungumza na Watumishi wa Sekretariet ya Tume hiyo.

Akizungumza na Watumishi wa Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama,  Naibu Waziri Sagini ameipongoza Tume kwa kuendesha mchakato wa upatikanaji wa ajira za Watumishi wa Mahakama ya Tanzania kwa njia ya kielekitroniki ambapo amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza uwazi na kupunguza malalamiko.

“Naipongeza Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuendesha zoezi la ajira kwa njia ya kielekitroniki, hatua hii itasaidia sana katika kuongeza uwazi na kupunguza malalamiko na kutokuwepo kwa upendeleo”, alisisitiza Mhe. Sagini.

Naibu Waziri huyo pia aliishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuiwezesha Tume ya Utumishi wa Mahakama kutekeleza vema majukumu yake hususan katika bajetti na upatikanaji wa nafasi za ajira ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania.

Akizungumzia Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya, Naibu Waziri Sagini ameshauri Kamati hizo kutenga fedha kwa ajili ya vikao vya kamati vilivyopo kwa mujibu wa Sheria vinavyotakiwa kufanyika mara nne kwa mwaka.

Alisema kuwa Wizara ya Katiba na Sheria itasaidia katika kuitangaza Tume ya Utumishi wa Mahakama na kutoa elimu kwa wananchi kwa njia mbalimbali ili waweze kufanya juu ya uwepo wa kamati zinazopokea malalamiko ya wananchi yanayohusu ukiukwaji wa maadili ya Maafisa Mahakama ili wazifahamu na kuzitumia.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa kuhusu utendaji kazi wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama, Tume itaendelea kutoa elimu kwa njia mbailimbali ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

“Tutaendelea kuelimisha Umma kuhusu uwepo wa Kamati zinazopokea malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa Maadili ya Maafisa Mahakama kwa njia mbalimbali ikiwemo vipindi vya Redio na Televisheni” alisisitiza Katibu wa Tume.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi. 

Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.