ONGEZEKO LA TAASISI WADAU KWENYE MAONESHO WIKI YA SHERIA FAIDA KWA WANANCHI: DKT. SIYANI


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani amesema ongezeko la ushiriki wa wadau kwenye Maonesho ya wiki ya Sheria ni faida kwa wananchi kwa kuwa wigo wa utoaji wa elimu nao utaongezeka.

Kamishna huyo wa Tume ameyasema hayo tarehe 28 Januari, 2025 alipotembelea mabanda ya Wadau mbalimbali yaliyopo katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kufanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.

“Nakiri kufurahishwa na muitikio mkubwa wa Taasisi ambazo ni Wadau muhimu wa Mahakama ya Tanzania katika Maonesho ya mwaka huu kwa kuwa ongezeko hili la wadau ni faida kwa wananchi katika kupatiwa elimu ya sheria na masuala mengine” alisema Dkt. Siyami.

Alisema kuwa kadri Taasisi zinavyozidi kuongeza kasi ya ushiriki wake kwenye Maonesho ya Wiki ya Sheria ndivyo zinavyozidi kutoa fursa kwa wananchi ya kupata elimu kuhusu haki zao na masuala mengine mbalimbali.

Akizungumzia kuhusu kaulimbiu ya Wiki ya Sheria, Jaji Kiongozi alisema eneo la Haki Madai ni muhimu kwa kuwa linawakutanisha pamoja Wadau wa Haki Madai ili waweze kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo.

“Eneo la haki madai linahusu wananchi moja kwa moja, mchakato wa Haki madai unakuwa rahisi sana pale ambapo Sayansi na Teknolojia inatumika na wadau wote,” ameeleza Mhe. Dkt. Siyani.

Aidha, ametoa wito kwa Wananchi wote tanzania kutembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria ambayo yanaendelea kufanyika nchi nzima ili waweze kupata elimu kuhusu taratibu za Mahakama na sheria ili waweze kuzifahamu haki zao.

Maonesho ya Wiki ya Sheria yanatarajiwa kukamilika tarehe 31 Januari, 2025 huku kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini kinatarajiwa kufanyika siku ya Jumatatu tarehe 03 Februari, 2025.