RAIS MSTAAFU KIKWETE AIPONGEZA MAHAKAMA KWA MABORESHO YA HUDUMA ZAKE


Na Selina Mlelwa na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa maberesho makubwa yanayoendelea kufanyika ndani ya Mhimili wa Mahakama husanu uboreshaji wa utoaji wa haki kwa wananchi.

Akizungumza Wakati wa Uzinduzi wa Wiki ya Sheria leo tarehe 25 Januari, 2025 jijini Dodoma, Rais Mstaafu huyo aliyataja maeneo ambayo Mahakama imepiga hatua katika maboresho ya huduma zake huwa ni pamoja na ujenzi wa majengo ya kisasa ya Mahakama kwa ngazi zote, matumizi ya Tehama na usogezaji huduma za Mahakama karibu zaidi na Wananchi.

Alisema hivi sasa Mahakama imejenga majengo yake ya kisasa katika ngazi zote kuanzia Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya, Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama kuu katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo jengo la Makao makuu ya Mhimili wa Mahakama ambalo awali halikuwepo.

“Awali tulikuwa na tatizo la ukosefu wa majengo ya Mahakama na pia katika maeneo mengine wananchi walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kimahakama, lakini sasa tunayo majengo ya mahakama katika maeneo karibu yote nchini” alisema.  

Kuhusu matumizi ya Tehama, Mhe. Dkt. Kikwete amekiri kufurahishwa na maboresha hayo ikiwa ni pamoja na matumizi ya mifumo ya kielektroniki hasa ule wa kuratibu na kusikiliza mashauri mahakamani (Electronic Case Management System).

“Haikuwa hivyo zamani na Waheshimiwa mnajua. Hakika maboresho yote haya yanayoendelea yanaakisi maana halisi ya maendeleo,” alisema Rais huyo mstaafu.

Aidha, Mhe. Dkt. Kikwete pia ameipongeza Mahakama kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya kisheria na pia kwa Kauli Mbiu nzuri ya wiki na siku ya sheria inayoonesha ni kwa namna gani Mahakama inatambua nafasi yake kama mmoja ya Mihimili ya nchi inayoweza kutoa mchango muhimu katika ustawi wa kiuchumi na kijamii wa Watanzania.

Kauli mbiu  ya Wiki ya Sheria kwa mwaka huu inasema “Tanzania 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.”

Amesema, kufuatia kauli mbiu hiyo anayo matumaini kuwa Mhimili wa Mahakama  utashiriki kikamilifu katika mchakato unaoendelea sasa wa kutoa maoni kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleao ya mwaka 2050.

Awali akimkaribisha Mgeni rasmi kuzungumza, Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alisema kauli mbiu ya wiki ya Sheria ya mwaka 2025 inalenga kuikumbusha Mahakama kujipanga ili itekeleze Dira yam mwaka 2050 na kuzihamasisha Taasisi za Haki Madai zijiweke katika utayari wa kufanikisha malengo makuu ya Dira hiyo.

“Tunakumbushana kuwa Mahakama, na pia Taasisi za Haki Madai, zina wajibu wa kuhakikisha kwamba, mfumo wa sheria na utawala bora unaohitajika utaakisi malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yanafikiwa kikamilifu,” alisema.

Kila mwaka Mahakama huadhimisha Siku ya Sheria ikiwa ni kuashiria mwanzo wa shughuli za Mahakama kwa mwaka husika baada ya kumalizika kwa likizo ya Mahakama inayoanza kila tarehe 15 Desemba na kumalizika tarehe 31 Januari.

Siku ya sheria nchini hutanguliwa na wiki ya sheria ambayo hutumika kutoa elimu ya sheria kwa wananchi kwa lengo la kuwawezesha kuelewa masuala mbalimbali ya kisheria ili wazifahamu haki zao.