RAIS SAMIA AAGIZA UTEKELEZWAJI MAPENDEKEZO YA JAJI MKUU


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaagiza Mawaziri wawili kusimamia utekelezaji wa haraka wa mapendekezo ya Jaji Mkuu wa Tanzania kuhusu kuiunganisha mifumo ya Tehama ya Taasisi za Haki jinai nchini.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo tarehe 1 Februari, 2024 wakati akihutubia kwenye Maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.

Rais Samia amewaagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Waziri wa Katiba na Sheria na Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) kushirikiana katika kutekeleza mapendekezo ya Jaji Mkuu wa Tanzania kuhusu kuiunganisha mifumo ya Tehama ya Taasisi za haki jinai nchini, matumizi ya Tehama na kuunda kamati ya pamoja ya wadau itakayopitia na kuandaa taratibu/hatua za utendaji kazi (business Process).

“Katika hotuba ya Jaji Mkuu, amebainisha maboresho makubwa ya Mahakama yaliyotokana na matumizi ya Tehama na ametoa mapendekezo yake kuwa Taasisi za Haki Jinai, nami nawaagiza Mawaziri kushirikiana na kutekeleza kwa haraka” alisisitiza Mhe. Samia.

Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama ya Tanzania katika kuboresha na kuimarisha shughuli za utoaji haki nchini. Aliongeza kuwa Serikali imekuwa ikiiwezesha Mahakama katika maeneo mbalimbali ikiwemo miundombinu ya majengo na kuongeza idadi ya watumishi wa Mahakama.

”Tumeongeza idadi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani kutoka Majaji 16 mwaka 2021 na kufikia Majaji 35 mwaka 2023 ambao ni sawa na ongezeko la asilimia 118, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka 63 mwaka 2021 na kufikia Majaji 105 mwaka jana sawa na ongezeko la asilimia 67”, alisema Rais Samia.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ametoa rai kwa Mahakama ya Tanzania kuona pia umuhimu wa kuimarisha mfumo wa haki madai nchini kwa kuwa upande huo nako kuna malalamiko ya ucheleweshwaji wa upatikanaji wa haki.

Aidha, Mhe. Rais ametoa wito kwa Majaji na Mahakamu nchini kusikiliza na kumaliza mashauri ya biashara kwa haraka ili kuimarisha na kulinda shughuli za biashara na uwekezaji.

”Upo uhusiano mkubwa kati ya haki na uwekezaji, Mwekezaji anathamini sana  muda kwa kuwa muda ni mali hivyo Mahakama hazina budi kujielekeza kupunguza muda wa mashauri mahakamani ili wawekezaji wa ndani na nje ya nchi muda wa uzalishaji”, alisema.

Akizungumzia suala la utendaji haki, Rais Samia amewataka Majaji na Mahakimu kutekeleza majukumu yao ya utoaji haki kwa kuwa Mahakama inalo jukumu la kikatiba la kutoa haki na kwamba kazi ya kutoa haki ni ya Mungu hivyo waifanye kwa uaminifu mkubwa na kutofungwa na masharti ya kiufundi.