RAIS SAMIA AMUAPISHA ALIYEKUWA KAMISHNA WA TUME KUWA JAJI WA MAHAKAMA YA RUFANI


Na Mwandishi-Mahakama, Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemwapisha aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.

Uapisho huo ulifanyika tarehe 15 Agosti, 2024 katika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Bunge na Mahakama, akiwepo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Hassan Zungu, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka.

Katika hafla hiyo, kulikuwepo pia na uapisho wa Viongozi wa Serikali, wakiwemo Mawaziri, Katibu Tawala wa Mkoa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali na Wakuu wa Taasisi.

Akizungumza baada ya uapisho wa Viongozi hao aliowateua jana tarehe 14 Agosti, 2024, Rais Samia alisema kuwa mabadiliko aliyoyafanya ni ya kawaida katika kuongeza ufanisi kwenye maeneo yao.

“Tunachotarajia kwenu ni kwenda kuongeza ufanisi kwenye maeneo yenu. Nendeni mkaishi viapo mlivyoapa na kufuata maadili ya kikazi yanayotakiwa,” alisema.

Mhe. Dkt. Samia aliwakumbusha wateule hao kuwa wakati wa kufanya kazi kuna utaalam waliousomea na kujiongeza kwa kutumia akili ya kawaida, hivyo akawasihi pale wanapoona inafaa wafanye hivyo katika kuwatumikia wananchi.  

Naye Makamu wa Rais, akiongea katika hafla hiyo, aliwaeleza Viongozi hao kuwa viapo walivyoapa mbele ya Rais na umma kwa ujumla ni vizito, hivyo akawasihi kuviishi katika nafasi zao.

“Matumaini ya Rais aliyewapa dhamana hiyo na Watanzania ni kwamba watapata huduma bora katika nafasi zenu mbalimbali. Kila mmoja aende akafanye kazi kwa bidii, mkashirikiane na Viongozi wengine ambao mtawakuta katika nafasi zenu ili kwa ujumla kama Taifa tuweze kwenda haraka zaidi,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwahimiza Viongozi hao kurejesha imani waliyoaminiwa na Rais kwa kuwajibika kwake na Taifa kwa ujumla. Aliwaeleza kuwa dhamana walizopewa ni kubwa, zinahitaji kujiamini, nidhamu na weledi.