RAIS SAMIA AZINDUA JENGO LA MAKAO MAKUU YA MAHAKAMA YA TANZANIA
Aipongeza Mahakama kwa kuwa na Mifumo inayosomana, azitaka Taasisi nyingine za Serikali kuiga
Na Mwandishi-Mahakama-Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 05 Aprili, 2025 ameweka historia kwa Mhimili wa Mahakama kwa kuzindua rasmi Jengo la kwanza la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania na kukiri kuwa jengo hilo la kisasa na la Kimataifa na lenye sifa na hadhi ya kuwa Makao Makuu ya Mhimili huo.
Uzinduzi wa jengo hilo ni hatua kubwa kwa historia ya Mahakama nchini kufuatia ukweli kwamba, Mhimili huo haukuwahi kuwa na jengo la makao makuu kwa kipindi cha miaka 104 tangu kuanzishwa kwake.
Akihutunia wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jengo hilo sambamba na uzinduzi wa Jengo la Ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na nyumba 48 za Makazi ya Majaji, Mhe. Dkt. Samia amesema kuwa, hatua ya upatikanaji wa jengo hilo ni moja ya maboresho makubwa yaliyofanyika ndani ya Mhimili wa Mahakama lengo likiwa ni kuboresha huduma ya upatikanaji haki.
“Leo tumeandika historia nyingine kubwa zaidi kwa upande wa Mahakama na ni zaidi ya ile ya awali ya uzinduzi wa majengo ya Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs) sita. Nimelikagua jengo hili kwenye baadhi ya Ofisi zikiwemo vyumba vya Magereza, Chumba maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa mbalimbali za Mahakama, Ofisi za Mawakili Watoto na nikiri kuwa lina kila sifa la kuwa Makao Makuu ya Mahakama,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia hakusita kuipongeza Mahakama ya Tanzania chini ya Uongozi wa Jaji Mkuu wa Tanzania kwa kuendelea kuwa mfano mzuri wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ambapo ameonesha kufurahishwa na Chumba maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa mbalimbali za Mahakama (Judiciary Visual Situation Room).
“Nimeona Chumba maalum cha Mifumo ya utoaji taarifa mbalimbali (Judiciary Situation Room) ambayo nimeambiwa ni ya pili kwa ukubwa duniani, kwakweli nimeshangazwa na yaliyomo ndani, tunayoyashuhudia leo ni matokeo ya tuliyashuhudia kwenye nchi za wenzetu,” amesema Mhe. Samia.
Ameongeza kuwa, Serikali inachukua suala la utoaji wa haki kwa uzito wa pekee na kwamba mpaka sasa jumla ya miradi 144 ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya ngazi mbalimbali za Mahakama unaendelea na kuahidi kuwa, miradi itakamilika kwa wakati.
Rais Samia, amebainisha kuwa kazi iliyofanywa na Mahakama ni zaidi ya kile kilichoahidiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCA) na Dira ya Taifa ya Maendeleo.
Kadhalika, Mhe. Dkt. Samia amesema kuwa, “Serikali itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi wake kadri uwezo wa kibajeti utakavyoruhusu.”
Kwa upande mwingine, amewakumbusha watumishi wa Mahakama kuimarisha utoaji wa huduma ya haki kwa wananchi na kugusia juu ya umuhimu wa Mahakama za Mwanzo kutofungwa na masharti ya kiufundi yanayozuia haki kutendeka kwa wakati.
Katika hotuba yake, Rais Samia amewasisitiza pia watumishi wa Mahakama kuhusu utunzaji wa miundombinu ya majengo ya Mahakama ambapo amekazia kwa kusema kwamba, “Jengo hili la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania na mengine niliyoyazindua nikipita hata baada ya miaka mitatu yawe hivihivi kwakuwa gharama za ukarabati ni kubwa.”
Ameikumbusha pia Mahakama kufanya maboresho ambayo pia yanazingatia Mahakama maalum mfano Mahakama ya Ardhi, Mahakama ya Masuala ya Familia na kadhalika.
Miradi mitatu iliyozinduliwa leo imegharimu kiasi ya fedha za kitanzania bilioni 185.4. Kupatikana kwa Jengo la Makao Makuu ya Mahakama kunafanya Mihimili yote mitatu ya Dola ikiwemo Serikali na Bunge kuwepo Makao Makuu ya Nchi jijini Dodoma.