RAIS SAMIA AZINDUA JENGO LA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA   


  • Tume yaandika Historia kuwa na Jengo lake

Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 05 Aprili, 2025 amezindua jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama na kuweka historia kwa Tume kuwa na jengo lake la ofisi tangu kuanzishwa kwake.

Sambamba na uzinduzi wa Jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama, Rais Samia pia amezindua jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania pamoja na nyumba 48 za makazi ya Majaji zilizopo eneo la Iyumbu mkoani Dodoma.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa majengo hayo, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Tume ya Utumishi wa Mahakama na Mahakama ya Tanzania katika kuimarisha shughuli za utoaji na kuboresha maslahi ya Watumishi wa Mahakama.

Alisema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha shughuli za utoaji kwa kuongeza idadi ya watumishi wa Mahakama wakiwemo Majaji na kuboresha maslahi ya watumishi hao lengo likiwa ni kuboresha mifumo ya utoaji haki nchini.  

“Serikali kwa upande wetu tumetekeleza jukumu letu kwenu watumishi wa Mahakama ya Tanzania na sasa tunadai ufanisi wa hali ya juu kutoka kwenu”, alisema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia alimpongeza Jaji Mkuu wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kazi iliyotukuka ikiwa ni pamoja na kufanya mageuzi makubwa mahakamani ikiwemo matumizi ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na ujenzi wa majengo bora na ya kisasa ya Mahakama nchini.

“Majengo haya bora na ya kisasa ya Mahakama ya Tanzania yaliyojengwa katika maeneo mbalimbali nchini hayana budi kuendana na huduma bora za utoaji haki kwa wananchi”, alisisitiza.

Aliwataka Majaji na Mahakimu kuwa waadilifu wanapotekeleza jukumu lao la  msingi la kutoa haki ili waweze kutenda haki na kulinda heshima ya Mhimili wa Mahakama.

 Rais Samia pia alimpongeza Jaji Mkuu kwa kukamisha ujenzi wa jengo la Ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama ambalo linaweka historia ya Tume kuwa na jengo lake tangu kuanzishwa kwake. Alisisitiza umuhimu wa kuyatunza majengo yote ili yaonekane bora wakati wote.

Awali akizungumzia miradi hiyo mitatu ya majengo yaliyozinduliwa, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel alisema fedha zilizotumika kukamilisha miradi yote hiyo zimetolewa na Serikali ya Tanzania.

Alisema majengo yote yaliyozinduliwa yamegharimu jumla ya shilingi bilioni 185.4. Akifafanua fedha hizo, Prof. Ole Gabriel alisema jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania lenye ghorofa tisa limegharimu kiasi cha shilingi bilioni 129.7 ambapo jengo la ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama limegharimu shilingi bilioni 14.3 huku nyumba za Makazi ya Majaji ziligharimu kiasi cha shilingi bilioni 41.4   

Alisema jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania lenye ghorofa tisa ni jengo la sita kwa ukubwa duniani na la kwanza barani Afrika kati ya majengo ya Mahakama. Jengo hili pamoja na mengine yaliyozinduliwa yamejengwa na kampuni ya CRJE (East Africa) Ltd.