RAIS SAMIA MGENI RASMI SIKU YA SHERIA NCHINI


  • Itatanguliwa na Wiki ya Utoaji Elimu kwa Wananchi

Na Lydia Churi - Tume ya Utumishi wa Mahakama

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi kwenye Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Sheria nchini, yatakayofanyika tarehe 03 Februari, 2025 jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameyasema hayo leo tarehe 14 Januari, 2025 jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Sheria.

Jaji M kuu alisema Siku ya Sheria nchini ambayo huadhimishwa kila mwaka  itatanguliwa na Wiki ya Sheria ambayo itakuwa ni wiki ya utoaji elimu kwa wananchi kuhusu Mahakama na masuala ya Sheria kwa ujumla ambayo pia itaambatana na Maonesho ya utoaji elimu yatakayoanza tarehe 25 Januari hadi tarehe 01 Februari mwaka huu katika maeneo mbalimbali yenye mkusanyiko wa watu jijini Dodoma na mikoa mingine nchini.

Aidha, Jaji Mkuu alisema kuwa hafla ya Siku ya Sheria nchini ’Law Day’ itafanyika kwenye Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atakuwa Mgeni Rasmi.

Akizungumzia uzinduzi wa Wiki ya Sheria, Jaji Mkuu alisema kuwa, Mgeni Rasmi anatarijiwa kuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambao utafanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere (Nyerere Square) Jijini Dodoma.

“Uzinduzi wa Wiki ya Sheria utatanguliwa na Mbio Maalumu (Fun Run) za kilomita 10 ambazo zitaambatana na matembezi ya umbali wa kilomita tano kwa wale ambao watapendelea kutembea. Katika hizo mbio maalum na matembezi ya tarehe 25 Januari 2025, tutaongozwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,” alieleza Mhe. Prof. Juma.

Akielezea namna maadhimisho hayo yatakavyofanyika nchini, Jaji Mkuu amebainisha kuwa, Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria yatafanyika katika ngazi ya Kitaifa, Kanda za Mahakama Kuu, Divisheni za Mahakama Kuu, Mikoa na Wilaya zote nchini ambapo elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria itatolewa katika maeneo mbalimbali.

“Maadhimisho ya Wiki ya Sheria ni jukwaa maalum linaloikutanisha Mahakama na wadau wake muhimu hususani wananchi ili kutoa elimu ya shughuli zinazotolewa na Mahakama na wadau wake walio katika mnyororo wa utoaji haki,” amesema Mhe. Prof. Juma.

Alifafanua kuwa zoezi la utoaji elimu litahusisha Majaji, Wasajili, Naibu Wasajili, Watendaji na Mahakimu na kwamba Mahakama itashirikiana na Wadau wake muhimu kama vile Tume ya Utumishi wa Mahakama, Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Tume ya Kurekebisha Sheria, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na  Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).

Taasisi nyingine zitakazoshiriki katika kutoa elimu ni Ofisi ya Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Chama cha Majaji Wanawake (TAWJA), Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na wadau wengine.

Aidha, Jaji Mkuu ameeleza kuwa, kwa kuzingatia kwamba maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanafanyika siku za kazi ambapo wananchi wengi wanakuwa kwenye shughuli za utafutaji wa kipato, utoaji elimu kwa mwaka huu umelenga kuwafuata wananchi karibu zaidi na maeneo yao wanayofanyia kazi tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

“Tutatoa elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi kwa kutumia magari maalumu yatakayokuwa yanahama kutoka eneo moja kwenda eneo jingine. Tutaongeza wigo wa utoaji elimu kwenye shule za msingi, sekondari na vyuo ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi,” amebainisha Mhe. Prof. Juma. 

Kadhalika, amesema kwamba ili kuhakikisha elimu inawafikia watu wengi wigo wa vipindi vya utoaji elimu kwenye vyombo vya habari kupitia luninga, redio na mitandao ya kijamii utaongezeka pia ambapo ameeleza kuwa, “Ni matumaini yetu kwamba utaratibu wa mwaka huu utatuwezesha kuwafikia wananchi wengi zaidi ambao wanahitaji kupata uelewa wa masuala mabalimbali ya kisheria.”

Kaulimbiu ya Wiki na Siku ya Sheria mwaka huu inasema, ‘Tanzania 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo’.

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini hufanyika kila mwaka  kuashiria mwanzo wa kuanza kwa shughuli za Mahakama kwa mwaka husika baada ya kumalizika kwa likizo ya Mahakama inayoanza kila tarehe 15 Desemba na kumalizika tarehe 31 Januari ya mwaka unaofuatia.