RC MTANDA ASHAURI WAKUU WA WILAYA KUTENGA FEDHA KUENDESHA VIKAO VYA KAMATI ZA MAADILI
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama-Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa Mhe. Said Mtanda amewashauri Wakuu wa wilaya mkoani humo kutenga fedha kwenye bajeti zao kwa ajili ya kuendesha vikao vya kamati za Maadili kwa kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria.
Mhe. Mtanda ameyasema hayo leo Tarehe 13 Mei, 2024 wakati akitoa neno la ufunguzi wa kazi ya utoaji Elimu kwa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama katika Mkoa wa Mwanza inayofanywa na Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama.
”Tayari maeneo mengine tulikuwa tukitenga fedha kwenye mgao wa OC kwa ajili vikao vya Kamati za Maadili kwa sababu hii ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria’’, alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza pia ameishauri Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na Mahakama ya Tanzania kushirikiana kwa karibu na Serikali hatua itakayosaidia kuziimarisha Kamati hizo na kuziwezesha kutekeleza majukumu yake ya kisheria.
”Tume ya Utumishi wa Mahakama tunaifahamu, tunaomba ushirikiano wenu wa dhati ili tuwe na uelewa wa pamoja katika shughuli za kila siku pamoja na kuziimarusha Kamati hizi’’, alisema Mhe. Mtanda.
Aidha, ametoa wito kwa Tume ya Utumishi wa Mahakama kuzihuisha kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa na Wilaya ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.
Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Maadili na Nidhamu) Bi. Alesia Mbuya alisema pamoja na mafunzo hayo, Watumishi wa Sekretariet ya Tume wamefika mkoani Mwanza kwa lengo la kuzihusisha Kamati hizo na kuanzisha ushirikiano kati yake na wajumbe wa Kamati hizo ili ziweze kufanya kazi zake ipasavyo.
Alisema, ili kuhakikisha wajumbe wa Kamati za Maadili wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi, wajumbe hao katika ngazi ya Mkoa na Wilaya hawana budi kusoma, kuelewa na kuzitumia Kanuni za Maadili pamoja na Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati hizo uliotolewa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na.4 ya mwaka 2011.