SERIKALI KUENDELEA KUIWEZESHA TUME KUSIMAMIA MAADILI  


Na Lydia Churi, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inaendelea kuiwezesha vema Tume ya Utumishi wa Mahakama ili iweze kusimamia kwa ufanisi maadili na nidhamu ya Watumishi wa Mahakama.

Rais Samia ameyasema hayo leo tarehe 03 Februari, 2025 wakati akiwahutubia watanzania kwenye Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini zilizofanyika katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.

“Napenda kukukumbusha Mhe. Jaji Mkuu kuwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025 tuliahidi pia kuiimarisha Tume ya Utumishi wa Mahakama ili iweze kusimamia kwa ufanisi maadili na nidhamu katika utumishi wa Mahakama”, alisema Rais Samia.

 Alisema Serikali inaahidi kuendelea kuyafanyia kazi maombi ya Tume ya Utumishi wa Mahakama ya kutetea maslahi ya Watumishi wa Mahakama.

Alisema Serikali inatambua kuwa mazingira ya kazi kwa Watumishi wa Mahakama ni magumu, ili haki  iweze kushamiri na maslahi  ya nchi na wananchii yalindwe vyema ni wajibu wa Serikali kutengeneza mazingira mazuri hivyo maombi yaliowasilishwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama yanaendelea kufanyiwa kazi hatua kwa hatua.

"Ni imani yangu kwamba mpaka sasa Serikali tumeshafanya vyema katika kuiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake, hayo maombi mengine yataendelea kufanyiwa kazi na Serikali, " Alisema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia alimshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume kwa kutambua mchango uuliotolewa na Serikali katika maboresho ya Muhimili wa Mahakama na kusema kuwa Serikali inafanya yote haya kwa kuwa inaamini katika haki ili haki itamalaki nchini.

 Akizungumzia mafanikio ya Mahakama ya Tanzania hususan katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimpongeza Jaji Mkuu wa Tanzania kwa Mahakama kuendelea kuwa kinara katika matumizi ya TEHAMA barani Afrika.

“Mahakama yetu imekuwa ni mfano wa kuigwa kwa uchapaji wa hukumu kwa haraka kutokana na matumizi ya TEHAMA“Alisisitiza.

Rais Samia pia ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa hatua kubwa za mageuzi ya mitazamo na tamaduni kwenye utoaji wa huduma  ambapo idadi ya wananchi  wanaoridhishwa  na huduma  za Mahakama imeongezeka kutoka  asilimia    61 mwaka 2015  na kufikia asilimia 88  mwaka 2023.

Siku ya Sheria nchini huadhimishwa kila mwaka ambayo huashiria kuanza kwa mwaka mpya wa Mahakama. Siku hii hutanguliwa na wiki ya utoaji wa elimu kuhusu masuala ya Sheria. Mwaka huu, Wiki ya sheria ilianza Januari 25 na kumalizika Februari 1, 2025