SHIMIWI YATAKIWA KUANDAA PROGRAMU MAALUM YA MICHEZO KWA WATUMISHI
SHIMIWI YATAKIWA KUANDAA PROGRAMU MAALUM YA MICHEZO KWA WATUMISHI
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Tanga
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ametoa wito kwa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) kuandaa programu maalumu ya michezo itakayozishirikisha Taasisi za Umma kushindana kila mwezi kwa lengo la kuendeleza michezo na kuinua ari ya watumishi wa Umma kufanya mazoezi kila siku.
Akifungua rasmi mashindano ya (SHIMIWI) yanayoendelea jijini Tanga Waziri huyo pia amewashauri viongozi wa shirikisho hilo kukutana na Serikali na kujadili njia bora ya kuendeleza mashindano hayo ikiwa ni pamoja na kuona uwezekano wa kuongeza muda wa ushiriki katika mashindano hayo.
Akifafanua kuhusu umuhimu wa kuwa na programu maalum ya mashindano ya SHIMIWI, Waziri Mhagama alisema watumishi wa Umma wakiongezewa muda wa kucheza watapata nafasi ya kuonyesha umahiri na vipaji vyao na pia itakuwa ni njia bora ya upatikanaji wa wachezaji wazuri katika ngazi ya vilabu na taifa kwa ujumla.
Aliongeza kuwa kuwa uwepo wa muda wa kutosha katika ushiriki wa watumishi kwenye mashindano hayo kutayafanya yawe na tija na kusaidia nchi kuwa na timu bora ambazo zinaweza kushindana kwenye medani za kitaifa kutoka katika watumishi wa Umma nchini.
Aidha, Waziri huyo aliishauri SHIMIWI kuwa karibu na vyama vya michezo kwa kuwa vina utalaamu wa kutosha utakaosaidia kupata ubobezi katika medani za michezo ya aina mbalimbali.
Waziri huyo mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma nchini aliwaagiza kuwaagiza waajiri wote kuwaruhusu watumishi kujiandaa kikamilifu na mashindano ya SHIMIWI kwani haipendezi kwa mwanamichezo kushiriki mashindano pasipo kujiandaa vya kutosha.
“Tumeshuhudia taasisi ziliwawezesha wanamichezo wao kupata mavazi nadhifu ya michezo na leo uwanja umependeza. Nitoe wito kwa taasisi ambazo hazikujiandaa vizuri mwakani zijitahidi kufanya hivyo,” alisema.
Aliwakumbusha watumishi kuongozwa na maadaili ya utumishi wa Umma kwa kuwa suala la maadili siyo la hiari bali ni lazima.
Naye Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Pauline Gekul aliwakumbusha wanamichezo kuwa michezo ni taaluma ambayo inahitaji nidhamu na weledi kama zilivyo taaluma zingine, hivyo aliwataka watumishi wanaoshiriki michezo hiyo kuitumia kama chachu ya kuleta upendo, mshikamano, amani na umoja kwa watumishi wote na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SHIMIWI Taifa Bw. Daniel Mwalusamba alisema michezo ya mwaka huu imekuwa na mwitikio mkubwa ukilinganisha na ya mwaka jana. Alisema mwaka jana timu 47 zilishiriki kwenye michezo hiyo iliyofanyika mkoani Morogoro lakini mwaka huu timu 63 zinazoshiriki. Mashindano ya SHIMIWI yanafanyika kwa mara ya 36 tangu yalipoanzishwa hapa nchini.