SPIKA WA BUNGE AZINDUA MFUMO WA UNUKUZI NA TAFSIRI WA MAHAKAMA
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson leo tarehe 27 Januari, 2024 amezindua mfumo wa Unukuzi na Tafsiri wa Mahakama ya Tanzania utakaorahisisha upatikanaji wa haki nchini.
Akizungumza mara baada ya kuzindua Mfumo huo ambao pia utaongeza uwazi kwenye shughuli za Mahakama, Dkt. Tulia amewataka wadau wa utoaji haki nchini kwenda na kasi ya Mhimili wa Mahakama katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na kushirikiana na Mhimili huo ili wananchi wapate haki kwa wakati na kwa urahisi.
”Tunatamani Mahakama inaposonga mbele kwa kasi katika matumizi ya Tehama, wadau pia wasonge mbele”, alisema Spika.
Alisema Mfumo wa Mahakama wa Unukuzi na Tafsiri unazitaka Taasisi zilizo kwenye mnyororo wa utoaji haki kufanya uwekezaji wa miundombinu ya Tehama kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania, kutoa mafunzo mbalimbali, kuwa na vifaa vya kisasa vya Tehama na wadau kuongeza ushirikiano ili wananchi wapate haki kwa wakati.
Aidha, Spika wa Bunge ambaye alikuwa Mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa wiki ya Sheria aliwakumbusha wadau kwenye mnyororo wa haki jinai kuwa ujenzi wa mifumo ya Tehama katika Taasisi zao uzingatie kuwa na uwezo wa kuunganishwa na mifumo mingine ili waweze kubadilishana taarifa za kiutendaji na kuongeza ufanisi katika kazi.
Awali akimkaribisha Mgeni rasmi kuzindua mfumo huo, Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alisema Mfumo wa unukuzi na tafsiri wa Mahakama utaleta mapinduzi makubwa katika suala zima la upatikanaji wa haki nchini.
”Mfumo huu ni mfano wa matumizi ya akili bandia (Artifial Intelligence), umeandaliwa kwa kuhusisha lafudhi zetu zote, tujivunie mfumo huu kwa kuwa ni zao linalotokana na kodi za Wananchi”, alisema Jaji Mkuu.
Akiuelezea Mfumo huo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel alisema mfumo wa Unukuzi na Tafsiri utatumia lugha ya kiswahili cha kitanzania na hasa cha kimahakama na lugha ya Kiingereza cha kitanzania cha kimahakama.
Alisema mfumo huu unaendana na mabadiliko ya sheria mbalimbali yaliyofanyika mwaka 2021. Aliongeza kuwa hivi sasa unafanya kazi kwa zaidi ya asilimia 90 ambapo haki miliki ni ya Mahakama na endapo nchi yeyote duniani ikitaka kuutumia italipa asilimia 20 ya faida inayopatikana kama maduhuli kwa serikali ambayo imeugharamia.
”Mfumo huu tayari umefungwa katika Mahakama 11 nchini vikiwemo vituo Jumuishi vya utoaji haki 6 vya Arusha, Mwanza, Dodoma, Morogoro, Kinondoni na Temeke pamoja na Mahakama Kuu Bukoba, Musoma, Divisheni ya Biashara na ile ya Makosa ya Rushwa na uhujumu Uchumi na Masjala ndogo ya Dar es salaam.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama alisema pamoja ya kuwa mfumo huu umetengenezwa na Mahakama, taasisi nyingine za umma zinaweza kuutumia. Aliongeza kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mahakama Kuu Zanzibar ni miongoni mwa taasisi zilizotembelea Mahakama na kujifunza kuhusu mfumo huo.
Alizitaja baadhi ya faida za mfumo huo kuwa ni pamoja na kuokoa gharama na muda pamoja na kuweka ushahidi wa uhakika wa sauti na maandishi.
Uzinduzi wa Wiki ya Sheria ulitanguliwa na matembezi yaliyooanzia kwenye Kituo Jumuishi cha Utaoji Haki Dodoma na kuishia kwenye viwanja vya Nyerere Square. Mgeni rasmi kwenye matembezi hayo alikuwa ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Akson.