TUME IKO MAKINI KUSIMAMIA MAADILI YA WATUMISHI WA MAHAKAMA: NAIBU KATIBU
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Iringa
Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Maadili na Nidhamu) Bi. Alesia Mbuya amesema Tume iko makini katika kusimamia maadili na nidhamu ya Watumishi wa Mahakama ili kujenga taswira chanya ya Mhimili wa Mahakama.
Naibu Katibu wa Tume ameyasema hayo leo mjini Iringa wakati alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa katika mafunzo yanayolenga kuimarisha utendaji kazi wa Kamati za Maadili za Mikoa na wilaya.
”Tume ya Utumishi wa Mahakama imedhamiria kusimamia kikamilifu maadili na nidhamu ya watumishi wa Mahakama hivyo watumishi hawana budi kufanya kazi kwa kuzingatia maadili,” alisema.
Alisema Tume inaendelea kuwachukulia hatua watumishi wa Mahakama wanaokiuka maadili ikiwemo kuwafukuza kazini wale wanaobainika kutenda makosa yanayostahili adhabu hiyo.
Aidha, alitoa wito kwa Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama Mkoa wa Iringa kuwaelimisha wananchi kuhusu uwepo wa Kamati hizo ili waweze kuzitumia kuwasilisha malalamiko yao yanayohusu ukiukwaji wa maadili kwa Mahakimu.
Alisema Tume kwa upande wake inaendelea na jitihada zake za kutangaza uwepo Kamati hizi kwa njia mbalimbali ikiwemo kupitia vyombo mbalimbali vya habari pamoja na kufanya mikutano na baadhi ya watendaji wa Serikali.
Naye Mjumbe wa Kamati hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa Mhe. Adelina Ngwaya ameshauri Tume kufanya kazi ya ulezi zaidi kwa Maafisa Mahakama kuliko kusubiri kutoa adhabu.
Aliiomba Tume ya Utumishi wa Mahakama kuboresha mazingira ya kazi kwa Mahakimu hususan kuwatafutia makazi bora ili wawe katika mazingira yatakayowazesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Kwa upande wake, Mjumbe mwingine wa Kamati Bw. Amani Mwamwindi aliishukuru Tume kwa kuwaandalia mafunzo ambapo alisema kuwa mafunzo waliyopata yatawasaidia kuimarisha utendaji wao wa kazi za Kamati.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.
Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia kwenye jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye Kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.