TUME KUSHIRIKI MAONESHO YA WIKI YA SHERIA DODOMA


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni miongoni mwa Taasisi  wadau wa Mahakama ya Tanzania zinazotarajiwa kushiriki Maonesho ya Wiki ya Sheria yatakayofanyika Januari 24-30, 2024 jijini Dodoma.

Maonesho ya Wiki ya Sheria yatafanyika kwenye viwanja vya Nyerere Square jijini humo na mwaka huu yataongozwa na Kaulimbiu  “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau Katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai.”

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza hivi karibuni kuhusu Wiki ya Sheria alisema  Maonesho hayo yatazinduliwa rasmi tarehe 27 Januari, 2024 kwa matembezi maalum yatakayoongozwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson.

“Maonesho haya yatazinduliwa kwa matembezi maalum yatakayoanzia Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Dodoma hadi Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini humo, matembezi haya yataongozwa na Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson,” alisema.

Jaji Mkuu alisema kuwa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Sheria kitafanyika tarehe 1, Februari 2024 katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alizitaja baadhi ya Taasisi wadau wa Mahakama zitakazoshiriki Maonesho hayo kuwa ni Tume ya Utumishi wa Mahakama, Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Mamlaka ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya, Ofisi ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na wengine. 

Aidha, Jaji Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ametoa wito kwa wananchi wote  kutembelea maonesho hayo ya Wiki ya Sheria ili kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu shughuli za utoaji haki.

”Ni muhimu wananchi na wadau kutembelea maonesho hayo kwa kuwa yatawawezesha kufahamu masuala mbalimbali ya kimahakama ikiwa ni pamoja na Uandishi wa Wosia, Usimamizi wa Mirathi na huduma nyingine. 

Alisema katika Maonesho hayo wananchi watapata fursa ya kuzungumza, kuuliza maswali na kujadiliana na Maafisa wa Mahakama na wadau wake kwa lengo la kujifunza kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Mahakama na pia zile zinazotolewa na wadau. 

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Tume imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011.