TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA YADHAMIRIA KUWAFIKIA WANANCHI
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Singida
Tume ya Utumishi wa Mahakama imedhamiria kuwafikia wananchi na kuwaelimisha kuhusu uwepo wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya zinazopokea malalamiko ya Wananchi yanayohusu ukiukwaji wa Maadili ya Maafisa Mahakama.
Akifungua mafunzo maalum ya siku mbili kwa Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Singida leo mkoani humo, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Maadili na Nidhamu) Bi. Alesia Alex Mbuya alisema mafunzo hayo yatawawezesha wananchi kufahamu uwepo wa Kamati hizo na kuwasilisha malalamiko yao.
Alisema Tume imeona ni muhimu kuwatumia Maafisa Tarafa kuwaelimisha wananchi kuhusu majukumu yake ikiwemo namna ya kuwasilisha malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa Maadili kwa Maafisa Mahakama kwa kuwa Maafisa Taarafa ni kiungo kati ya Serikali na Wananchi katika Tarafa na ni wawakilishi wa Wakuu wa Wilaya katika shughuli za kijamii, miradi ya maendeleo na katika kutatua migogoro ya wananchi.
”Moja ya mikakati ya kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwaelimisha ni kwa kuwatumia ninyi Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Singida lengo likiwa ni kuwaelimisha ninyi ili nanyi mkawaelimishe wananchi hasa mnapokutana nao kupitia fursa mlizonazo mnapotekeleza majukumu yenu ya kila siku kwa wananchi”, alisema.
Naibu Katibu alisema kuwa mafunzo hayo ni moja ya utekelezaji wa misingi ya utawala bora ya Tume unaozingatia Sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mkoa na Wilaya.
Alisema, ni matarajio ya Tume kuwa, kupitia mafunzo hayo Maafisa Tarafa wataisaidia Tume kuwaelimisha wananchi namna ya kuwasilisha malalamiko yao kwa njia sahihi ili waweze kupata haki kwa wakati.
Alizitaja Mada zitakazotolewa kwenye mafunzo hayo kuwa ni Tume ya Utumishi wa Mahakama, Muundo na Majukumu yake, Kanuni za Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya na uwasilishaji wa malalamiko pamoja na Mgawanyo wa majukumu kati ya Mihimili ya Dola.
Aidha, aliwasisitiza Maafisa hao kuzingatia maadili ya Uongozi katika Utumishi wa Umma na kujiepusha na vitendo vya rushwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhusiano mwema na wananchi wanaofika kupata huduma kwenye maeneo yao.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ilitoa mafunzo kama haya mwezi Juni mwaka huu kwa kwa Maafisa Tarafa 23 wa Mkoa wa Arusha.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.