TUME YAFANYA USAILI WA WATUMISHI WA MAHAKAMA KWENYE MAENEO MBALIMBALI NCHINI


Na Mwandishi-Tume ya Utumishi wa Mahakama

Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama leo imeanza zoezi la Usaili wa waombaji wa nafasi za ajira ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania katika maeneo mbalimbali nchini kufuatia tangazo la ajira lililotolewa tarehe 3 Juni, 2025.

Usaili huo wa awamu ya kwanza unaofanyika kwa njia ya kielekitroniki umeanza leo tarehe 19 Julai, 2025 na unatarajiwa kumalizika tarehe 26 Julai, 2025 katika maeneo mbalimbali ambapo Wasailiwa hawalazimiki kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kufanya usaili, badala yake wanafanya katika maeneo ya karibu. Lengo likiwa ni kuwapunguzia gharama waombaji wa nafasi za kazi waliojitokeza.

Aidha, usaili huo unafanyika kwenye maeneo mbalimbali nchini yakiwemo Arusha, Moshi, Kigoma, Tanga, Dodoma, Geita, Musoma, Mbeya, Morogoro, Mtwara na Mwanza. Maeneo mengine ni pamoja na Bukoba, Iringa, Sumbawanga, Katavi, Songea, Shinyanga  na Tabora.

Kwa mujibu wa Tangazo la uwepo wa nafasi za Ajira kwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania, nafasi zilizotangazwa ni kwa kada za Hakimu Mkazi ll, Afisa Utumishi, Afisa Mwendesha Ofisi, Mwandishi Mwendesha Ofisi, Mkutubi, Msaidizi wa Maktaba, Msaidizi wa Hesabu na Msaidizi wa Kumbukumbu.

Kada nyingine ni Opareta wa Kompyuta, Opareta wa Kompyuta Msaidizi, Msaidizi wa Ofisi, Mlinzi, Mpishi, Dereva na Technicians (Plumber, Air Condition, Carpenter, Electrical, Painter, Welding).  

Mamlaka ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kama chombo cha kusimamia ajira na nidhamu za watumishi wa Mahakama yanatokana na Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na kifungu Na. 29 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama sura ya 237.