UJENZI JENGO LA TUME DODOMA WAFIKIA ASILIMIA 96


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Ujenzi wa jengo la Ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama unaoendelea jijini Dodoma unaelekea ukingoni ambapo hivi sasa jengo hilo limefikia asilimia 96 ikiwa ni hatua ya umaliziwaji wa jengo hilo.

Jengo hilo la Ofisi za Tume linajengwa kwenye kiwanja namba 3 Block D katika eneo la NCC, pembeni ya jengo la makao makuu ya Mahakama ya Tanzania.

Aidha kiwanja kinachotumika kujenga jengo hilo kina ukubwa wa mita za mraba 9,590, na kina hati yenye namba DOM008194 iliyotolewa tarehe 22 Julai, 2022.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Ugavi cha Tume ya Utumishi wa Mahakama, Jengo hilo linatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi Bilioni 14.3 (14,300,000,000) na Mzabuni wa jengo hilo ni CRJE (EAST AFRICA) LTD.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi. 

Tume ya Utumishi wa Mahakama imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.