‘VYOMBO VYA HABARI DARAJA MUHIMU KWA MAHAKAMA NA WANANCHI’


Na Faustine Kapama– Mahakama, Lindi

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amesema vyombo vya habari ni daraja muhimu baina ya Mahakama na wananchi, hivyo vinapaswa kushiriki katika kujenga taswira chanya ya Mahakama kwa kuuhabarisha umma kuhusu mambo mazuri yanayotokea mahakamani ili kukuza imani ya wananchi.

Mhe. Siyani ameyasema hayo katika siku ya pili ya ziara ya Tume ya Utumishi wa Mahakama chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambayo leo tarehe 21 Juni 2022 imetembelea Mkoa wa Lindi kuzungumza na watumishi na wadau wa Mahakama.

“Vyombo vya Habari ni daraja muhimu baina ya mahakama na wananchi. Msiishie kukosoa mambo yanapokwenda mrama, lakini tusemeeni kwa kuyatangaza zaidi mazuri yanayofanywa na Mahakama zetu ili kujenga na kukuza imani ya wananchi kwa vyombo hivi vya haki,” amesema.

Mhe. Siyani amesema vyombo vya habari ni wadau wakubwa wa Mahakama na katika kutimiza jukumu lake la kutoa haki, ni lazima wananchi inayowahudumia wawe na imani na chombo hicho na wanapaswa kufahamu juhudi zinazofanywa na Mahakama katika kuboresha huduma zake za kutoa haki.

Kwa mujibu wa Mhe. Siyani, vyombo vya habari vina mchango wa kujenga taswira ya Mahakama kwa umma ambapo dhamira ya vyombo hivyo kupitia kazi zao inaweza kujenga picha chanya au hasi kwa Mahakama.

Aliotoa mfano kuwa kama vyombo vya habari vitajikita kuandika mabaya pekee, imani ya wananchi itashuka na hilo likitokea Mahakama itapoteza uhalali wa uwepo kwake na watu wataamua kujichukulia sheria mkononi. Hakuna mtu atakayekuwa salama kuishi kwenye nchi ambayo watu wake wanajikulia sheria mkononi,” ameonya Jaji Kiongozi.

“Kwa hiyo, bila kuathiri uhuru wa vyombo hivi katika kutoa habari zinazofichua uovu kwa lengo la kurekebisha na kuboresha, matarajio yetu pia kuwa vyombo vya habari vitatumia nafasi yake kushiriki katika kujenga taswira chanya ya Mahakama kwa kuuhabarisha umma kuhusu mambo mazuri yanayotokea mahakamani ili kukuza imani ya wananchi kwa mahakama zao,” amesema.

Jaji Kiongozi pia alizungumzia kuhusu Ofisi ya Mwendesha Mashtaka ambapo Mkurugenzi wa Mashtaka na wote wanaofanya kazi chini yake wanapaswa kuongozwa na misingi iliyowekwa na Katiba ya nchi kupitia ibara ya 59B (4) ambayo ni kutenda haki, kutokutumia madaraka vibaya, kuzingatia maslahi ya umma. Amesema hayo ni mambo ambayo kila anayefanya kazi chini ya ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka anapaswa kuyaishi.

“Mahakama inatarajia kwamba ofisi ya Taifa ya Mashtaka itafanya kazi kwa kuzingatia misingi hiyo na kama hilo litafanyika na kwa kuwa ofisi hii ndiyo inayosimamia upelelezi wa makosa ya jinai, basi hakutakuwa na mlundikano wa mahabusu wa muda mrefu magerezani. Aidha kukamilika kwa upelelezi ndani ya muda mfupi kutawezesha Mahakama pia kusikiliza mashauri husika kwa kasi,” amesema.

Jaji Kkongozi pia amewataja Afisa Huduma kwa Jamii kuwa ni mdau muhimu katika kupendekeza adhabu mbadala kwa watuhumiwa waliotiwa hatiani kwa makosa ambayo adhabu husika ni chini ya miaka mitatu kama inavyobainishwa katika kifungu 3(1) (4) cha Sheria (the Community Services Act (Cap. 291 R.E. 2019).

Amesema maafisa huduma kwa jamii wana jukumu la kuwasilisha uchunguzi wa kijamii wa watuhumiwa ambao wanastahili adhabu mbadala kwa makosa ya jinai kabla ya adhabu husika kutolewa kwa mujibu wa kifungu 3(1)(4) cha Sheria (the Community Services Act (Cap. 291 R.E. 2002).