WAENDESHA MASHTAKA WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA MASLAHI YA UMMA


Na Lydia Churi- Mahakama, Morogoro

Tume ya Utumishi wa Mahakama imetoa wito kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kutekeleza majukumu yake kwa kuongozwa na dhamira tatu ambazo ni kutenda haki, kutotumia madaraka vibaya na kuzingatia maslahi ya Umma.

Akizungumza katika Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na wadau uliofanyika jana mjini Morogoro, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani amesema endapo ofisi hiyo itafanya kazi kwa kuzingatia misingi aliyoitaja, hakutakuwa na mlundikano wa mahabusu magerezani na upelelezi utakamilika kwa haraka kwa kuwa Waendesha mashtaka ndiyo wenye jukumu la kusimamia upelelezi wa makosa ya jinai nchini.

Jaji Kiongozi ambaye pia ni Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama amesema kuwa kukamilika kwa upelelezi wa makosa ya jinai kwa muda mfupi kutaiwezesha Mahakama kusikiliza mashauri kwa haraka zaidi na hivyo wananchi kupata haki kwa wakati.

“Mahakama inatarajia kuwa Waendesha Mashtaka watakapofanya kazi yao kwa weledi na kwa kuzingatia Sheria, taratibu na miongozo iliyopo, wataisaidi Mahakama kutenda haki”, alisema.

Alisema Waendesha Mashtaka wanatakiwa kuwa na ujuzi wa kutosha wa Sheria na kuwa na uwezo wa kuamua juu ya hatua ya mashauri wanayoyaendesha ikiwa kuna sababu ya kuendelea nayo au kuyaondoka mahakamani na hivyo kusaidia haki kupatikana kwa wakati.

Jaji Kiongozi alisema Mahakama inatarajia kuona Waendesha Mashtaka wakichukua hatua thabiti kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao na hivyo kutokukwamisha kasi ya usikilizwaji wa mashauri ya jinai mahakamani.

Aliwataka kufanya uamuzi kabla ya kufikisha shauri mahakamani badala ya kulifikisha likiwa na mapungufu mengi ya kisheria na kiushahidi. Alifafanua kuwa uamuzi wa kulifikisha shauri mahakamani uzingatie uwepo wa ushahidi wa kutosha.

Kuhusu Maafisa Ustawi wa Jamii ambao pia ni wadau muhimu katika usikilizwaji wa mashauri, Jaji Siyani Mahakama inatarajia kuwa Maafisa Ustawi wa Jamii watakuwa chachu ya kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa haki na si kikwazo

Alisema Maafisa hao hawana budi kuwepo mahakamani kwa kuwa wanayo nafasi kubwa katika kuharakisha usilikilizwaji wa mashauri yanayowahusu watoto. Aliongeza kuwa Maafisa hawa wasipokuwepo mahakamani hukwamisha shughuli za usikilizwaji wa mashauri ya watoto.

Kwa upande wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea (TLS), Mhe. Siyani alisema wanalo jukumu la kuisaidia Mahakama kutenda haki kwa kuwa uwepo wao mahakamani unausaidia Umma kufikia huduma za Mahakama na hivyo haki kupatikana kwa wakati.

Aidha, ametoa rai kwa Mawakili kuwashauri wateja wao kutumia usuluhishi kama njia ya kutatua migogoro yao kwa lengo la kupunguza gharama na kujenga jamii yenye mshikamano, undugu na kudumisha Amani.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Martine Shigela ameahidi kuendeleza kushirikiano uliopo kati ya Mhimili wa Mahakama na Serikali mkoani Morogoro ili kuwezesha wananchi kupata haki kwa wakati.

Mkuu huyo wa Mkoa ameipongeza Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuandaa Mikutano na wadau wa Mahakama pamoja na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama za wilaya na Mkoa kwa lengo la kutoa elimu na kubadilishana uzoefu ili kuboresha mazingira ya utoaji haki nchini.

Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaendelea na ziara katika mikoa ya Morogoro na Tanga baada ya kumaliza ziara katika mkoa wa Pwani. Ziara hiyo ya Tume ina madhumuni ya kuitangaza Tume hiyo, kutoa elimu na kukutana na wajumbe wa Kamati za Maadili za mikoa na wilaya pamoja na wadau wa Mahakama ili kuboresha huduma zinazotolewa na Mahakama.