WAJUMBE WA TUME WAKUTANA JIJINI DAR ES SALAAM
Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama
Tume ya Utumishi wa Mahakama imekutana katika kikao chake cha robo ya kwanza ya mwaka ambapo pamoja na mambo mengine, imefanya uamuzi kwa mashauri ya kinidhamu ikiwemo baadhi ya watumishi kupewa onyo, kufutiwa makosa na wengine kufukuzwa kazi kwa yale makosa yanayohitaji adhabu ya kufukuzwa kazi.
Akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kati ya taarifa zilizowasilishwa kwenye kikao hicho mojawapo ilihusu mashauri ya kinidhamu ya watumishi wa Mahakama.
Alisema kuwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania hawana budi kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa kuzingatia maadili mema ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi wanaofika mahakamani kutafuta haki zao.
”Ifahamike kwamba Tume haina mchezo na masuala ya nidhamu, uwajibikaji na pale ambapo Mtumishi anakutwa na hatia, hatua kali zinachukuliwa ikiwemo kuachishwa kazi kwa maslahi ya Umma”, alisisitiza.
Aidha, Katibu huyo wa Tume alitaja taarifa nyingine iliyowasilishwa kwenye kikao cha Tume kuwa ni kuhusu maslahi ya watumishi wa Mahakama. Alieleza kuwa maombi ya kuboreshwa kwa maslahi ya watumishi wa Mahakama tayari yamewasilishwa serikalini na hivi sasa yanafanyiwa kazi.
Mambo mengine yaliyojadiliwa na Wajumbe wa Tume ni pamoja na michakato ya uteuzi na ajira ndani ya Mahakama, upandishwaji vyeo na kubadilishwa Kada kwa watumishi, mchakato wa nafasi za ajira walizopatiwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Aidha, aliishukuru kwa kutoa nafasi 329 za ajira wa Mhimili wa Mahakama.
Kuhusu Tume kuhamia Dodoma, Katibu wa Tume alisema jengo la ofisi za Tume limeshakamilika kwa asilimia 98 na kwamba ifikapo Januari, 2025, Watumishi wa Tume watahamia jijini Dodoma.
Katika hatua nyingine, Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wamekipongeza Kituo cha Huduma kwa Wateja (call centre) cha Mahakama ya Tanzania kwa utendaji kazi mzuri tangu kuanzishwa kwake Machi Mosi mwaka 2023 ambapo asilimia 98.3 ya malalamiko yaliyopokelewa yameshughulikiwa.
Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama walikutana mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaam katika kikao chao kilichopo kwa mujibu wa Sheria ambapo hukutana mara nne kwa mwaka yaani kila robo ya mwaka. Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma jijini Dar es salaam.