WATUMISHI WA TUME WATAKIWA KUFANYA KAZI ZINAZOONESHA MATOKEO


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka watumishi wa Tume hiyo kufanya kazi kwa kujituma, kuongeza uwajibikaji wenye tija katika kutoa haki na kutumia taaluma zao kufanya kazi zinazoonesha matokeo.

Akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Sekretarieti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama na kuzindua baraza hilo leo katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es salaam, Mwenyekiti huyo wa Tume pia amesisitiza masuala mengine matano muhimu ambayo watumishi wa Tume hiyo wanapaswa kuyazingatia wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.

Alisema licha ya kuongeza uwajibikaji na kujituma, watumishi hao wanapaswa kuzingatia matumizi ya Tehama ambayo yamerahisisha shughuli za utoaji haki. Alisema Mahakama ya Tanzania imefanya uboreshaji wa huduma zake kwa makusudi kutoka kutumia TEHAMA kama nyenzo ya kusambazia taarifa au habari mpaka kufanya TEHAMA kuwa nyenzo muhimu kwenye utendaji kazi wa kila siku za utoaji haki kwa wananchi.

“Uboreshaji wa huduma unaoendelea ndani ya Mahakama ukawe chachu kwa Sekreterieti ya Tume kuwezesha kazi za Sekreterieti na za Tume kuweza kufanywa kwa kutumia TEHAMA, kwa mfano katika utunzaji wa kumbukumbu na taarifa katika mikutano ya Tume na Kamati zake zipunguze au kuondoa kabisa matumizi ya karatasi”, alisema.  

Ubunifu kwa watumishi wa Sekreterieti ni jambo la tatu alilosisitiza Mwenyekiti huyo wa Tume kwa watumishi. Aliwataka kuwa wabunifu katika kazo zao ili kuiwezesha Tume kutimiza wajibu wake wa Kikatiba na Kisheria. Aliongeza kuwa ubunifu ni lazima ujengwe kutokana na misingi imara ya uelewa wa kina wa vifungu vya Katiba, sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali vinavyoogoza Taasisi hiyo

“Ubunifu unaongezwa kwa kujisomea, kujitafutia taarifa na kujiongezea ujuzi pia kwa kujifunza kutoka Tume nyingine zenye viwango vya ubora”, alisisitiza Jaji Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume hiyo.

Jambo la nne alilosisitiza Prof. Juma ni watumishi kuwa na maadili mema kwa kuwa Tume ya Utumishi wa Mahakama imepewa jukumu la Kikatiba la kusimamia maadili na nidhamu. “matarajio ya Tume ya Utumishi wa Mahakama ni kuwa na watumishi wa Sekreterieti ya Tume hiyo wenye maadili yasiyotiwa shaka, itakuwa ni kichekesho pale Tume inapohubiri maadili huku watumishi katika Sekretarieti wakikosa maadili”, alisema.

Utunzaji wa siri za ofisi ni ni jambo la tano alilosisitiza Jaji Mkuu kwa watumishi wa Tume hiyo. Alisema Sheria ya Usimamizi wa Mahakama, Namba 4 ya mwaka 2011 imesheheni vifungu kadhaa vinavyosisitiza umuhimu wa kutunza siri za ofisi. Kifungu cha 16 (1) cha Sheria hii, kinahusu wajibu wa Makamishna, Katibu na Naibu Katibu kuapa mbele ya Mwenyekiti kabla ya kuanza shughuli za Tume. Kifungu kidogo cha (2), kimempa Mwenyekiti mamlaka ya kumtaka mtumishi yoyote katika Sekreterieti ya Tume, kula kiapo kwa mujibu wa Jedwali ya Tatu ya Sheria hiyo.

“Msisitizo wa vifungu vya sheria ni kumbusho kwa Watumishi kuwa, ni kinyume cha sheria, kwa mtumishi wa Tume kutoa taarifa yoyote ya Tume kwa mtu asiyehusika bila kibali ama kuzingatia taratibu. Aidha, ninaweka mkazo katika suala zima la utii wa kazi, kwa viongozi na pia kuheshimiana. Haya yote yakizingatiwa utendaji utakuwa ni wenye tija”, alisisitiza Mwenyekiti huyo wa Tume.

Jambo la sita lililosisitizwa na Jaji Mkuu ni watumishi wa Tume kujiandaa kisaikolojia kuhamia Makao Makuu ya nchi-Dodoma mwezi Julai, mwaka huu. Aliwashauri watumishi hao kufanya maandalizi yote muhimu ya kuhamia Dodoma ili muda utapowadia wahamie na kuendelea na shughuli za utoaji haki kwa ufanisi zaidi. Ujenzi wa jengo la Tume unaendelea mjini Dodoma na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni mwaka huu.

Aidha Mwenyekiti wa Tume aliwataka watumishi hao kutumia mkutano huo wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kujadili malengo na mipango ya taasisi huku akisisitiza tija na maslahi kuwa na uwiano ili kuleta matokeo ya utendaji kazi bora unaolenga kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Aliwataka kuwa vyanzo vya mawazo mapya na muelekeo mpya na huduma.

Awali akimkaribisha kuzindua Baraza hilo, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel alimweleza Prof. Juma kuwa katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku, watumishi wa Sekretarieti ya Tume huongozwa na Dira ya Tume ambayo ni kuwa kitovu cha ubora katika kusimamia watumishi wa Mahakama Tanzania Bara. Aidha, alisema watumishi hao wanaongozwa na Dhima ya Tume ambayo ni utoaji endelevu wa huduma ya ushauri na usimamizi wa rasilimali watu katika utumishi wa Mahakama Tanzania Bara.

Alisema kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 Sekretarieti ya Tume imejiwekea malengo ambayo yatasaidia kufanikisha majukumu yake, ikiwemo uwezeshaji wa maadili katika Mahakama ya Tanzania unaboreshwa na kuimarisha huduma za utawala bora katika Tume ya Utumishi wa Mahakama.

“Kwa hiyo, kimsingi tunajitahidi kuhakikisha kuwa utawala bora unakuwepo na pia mpango mkakati wa kuzuia rushwa unatekelezwa kwa ufanisi. Kama mnavyofahamu katika shughuli za watumishi wa Mahakama masuala ya maadili na kupambana na rushwa ni jambo la msingi sana,” alisema.

Prof. Ole Gabriel alieleza pia kuwa katika kipindi cha Julai 2022 hadi Disemba 2022 Sekretarieti ya Tume imefanikiwa kutekeleza majukukumu yake, ikiwemo kuwezesha Tume kufanya vikao vitatu na katika masuala mbalimbali kama uteuzi wa Majaji 22 wa Mahakama Kuu na Msajili wa Mahakama ya Rufani, kuthibishwa kwenye uongozi na ajira katika masharti ya kudumu kwa baadhi ya watumishi na kusimamia nidhamu na maadili.