WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA AKUTANA NA WATUMISHI WA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA NA MAHAKAMA


  • Awataka kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Maadili

Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Juma Homera ametembelea ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na Mahakama ya Tanzania na kuwataka watumishi wa Taasisi hizo kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia nidhamu na maadili.

Ziara ya Waziri Homera ambaye aliambatana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Zainabu Katimba pamoja na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Franklin Rwezimula imefanyika leo tarehe 25 Novemba, 2025 ambapo walikutana na Wajumbe wa Menejiment za Tume ya Utumishi wa Mahakama na Mahakama ya Tanzania pamoja na Watumishi wa Taasisi hizo.

Waziri wa Kattiba na Sheria ameahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa Viongozi na Watumishi wote wa Tume na Mahakama ili kuhakikisha wanatekeleza ipasavyo majukumu yao.

Akizungumzia Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya, Waziri Homera ametoa rai kwa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kushirikiana kattika kuandaa vikao ilivyopo kisheria ili kuweza kusimamia ipasavyo maadili na nidhamu za Maafisa Mahakama pamoja na watumishi wengine wa Mahakama.

Aidha, Waziri wa Katiba na Sheria aliwapongeza na kuwashukuru watumishi wa Tume na Mahakama kwa kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza ipasavyo jukumu lake la msingi la utoaji haki yake ikiwemo  usikilizaji wa mashauri.

“Nawapongeza sana kwa kazi kubwa mnayofanya hususani kazi ya kusikiliza mashauri na kumaliza kwa kipindi kifupi tofauti na zamani ambapo shauri lilikuwa likichukua muda mrefu sana kumalizika”, alisema Waziri Homera.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel alimueleza Waziri kuwa  Tume ya Utumishi wa Mahakama ni Taasisi ya kwanza nchini kutumia mfumo wa kielekitroniki katika usaili wa waombaji wa nafasi za kazi Mahakama ya Tanzania.

Kuhusu Usimamizi wa Maadili ya Watumishi wa Mahakama hususan Maafisa Mahakama (Mahakimu), Katibu wa Tume alisema hivi sasa Tume iko mbioni kuanza kutumia mfumo wa kielekitroniki utakaorahisisha kazi ya usimamizi wa maadili ya Watumishi wa Mahakama.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mahakama sura ya 237 kwa lengo la kusimamia Uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania

Mamlaka ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kama chombo cha kusimamia ajira na nidhamu za Watumishi wa Mahakama yanatokana na Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.