WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA ATEMBELEA MAONESHO WIKI YA SHERIA


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Damas Ndumbaro ametembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma na kusisitiza matumizi ya usuluhishi kama njia ya kutatiua migogoro   katika jamii.

Waziri wa Katiba alisema utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi unasaidia kumaliza shauri kwa haraka na kwa gharama nafuu na kuacha pande zote mbili zilizomaliza mgogoro kuwa na furaha na mahusiano mazuri.

“Wizara inawaomba wananchi na wadau mbalimbali watumie fursa hii ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya ususluhishi “, alisisitiza.

Alisema Wizara ya Katiba na Sheria imejipanga katika kusajili wasuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA),

“Huitaji kufika ofisini pale Mtumba, popote ulipo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania n ahata nje yake ili kujisajili, ingia kwenye tovuti ya wizara na kujaza fomu husika, tutashughulikia na kukutumia cheti chako kwa njia ya mtandao”, alisema Mhe. Ndumbaro.

Alisema hivi kuna Taasisi ya Utatuzi wa migogoro kwa njia Mbadala Tanzania (Tanzania Arbitration Centre) iliyoanzishwa hivi karibuni ambapo amewataka watanzania hasa wanaojihusisha na biashara na uwekezaji kuitumia Taasisi hiyo.

Maonesho ya wiki ya Sheria yanafanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma tarehe 22 Januari, 2023 na yatamalizika Januari 29, 2023. Aidha siku ya Sheria nchini itafanyika Tarehe 1 Februari, 2023 na Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo atakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluihu Hassan.