BUNGE LAIDHINISHA BILIONI 774.7 KWA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KWA MWAKA 2026/2027
Bunge la Tanzania limeidhinisha jumla ya shilingi Bilioni 774,789,136,714 kwa Wizara ya Katiba na Sheria, Taasisi zake pamoja na Mahakama ya Tanzania ambapo fedha hizo zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Miradi ya Maendeleo katika mwaka wa fedha wa 2026/2027.
Bunge limeidhinisha kiasi hicho cha fedha baada ya Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Homera kuwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Katiba na Sheria, Taasisi zake pamoja na Mahakama ya Tanzania kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027, tarehe 24 Aprili, 2026 jijini Dodoma,
Akizungumza wakati wa kuwasilisha mpango huo, kwa upande wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dkt Homera alisema Tume ina jukumu la msingi katika kusimamia rasilimali Watu ndani ya Mahakama hususan katika masuala ya Ajira na Uteuzi, Nidhamu na Maadili ya Watumishi.
Alieleza kuwa katika kutekeleza majukumu hayo Tume inalenga kuwa na Watumishi wa Mahakama wenye Weledi, Uadilifu, Uwajibikaji na wanaozingatia Utawala bora.
Aidha, Tume iliajiri watumishi 1,117 kati yao 173 ni Mahakimu Wakazi na 944 ni Watumishi wa Kada mbalimbali. Vilevile Watumishi 755 walipandishwa vyeo vya kimuundo.
Waziri Homera alisema kuwa Tume imefanya uteuzi wa kujaza nafasi nane (8) za viongozi mbalimbali kwa ajili ya Mahakama ikiwemo Wakuu wa Vitengo wawili (2) na Wakurugenzi wasaidizi sita (6).
Waziri wa Katiba na Sheria aliliambia Bunge kuwa Tume ya Utumishi wa Mahakama iliwathibitisha kazini jumla ya watumishi 114 wa kada mbalimbali.
Katika kuhakikisha maadili na nidhamu kwa watumishi wa Mahakama yanasimamiwa ipasavyo, Tume ilishughulikia mashauri ya nidhamu ya Maafisa Mahakama na wasio Maafisa Mahakama na kutolewa uamuzi.
Kuhusu kuimarisha Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya, Dkt. Homera alisema Tume imefanya ufuatiliaji katika Mikoa ya Geita na Kagera na Wilaya zake kwa lengo la kuangalia namna Kamati zinavyotekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama na kushauri juu ya uendeshaji wa Kamati hizo.
Hotuba hiyo imewasilishwa kama sehemu ya ratiba ya Serikali ya kuwasilisha mipango na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ambapo utekelezaji wake unatarajiwa kuanza Julai 1, 2026.

