NAIPONGEZA SERIKALI KWA KUTOA KIPAUMBELE KWA MAHAKAMA YA TANZANIA : PROF. OLE GABRIEL
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel ameipongeza Serikali kwa kutoa kipaumbele kwa Mahakama ya Tanzania katika uwekezaji wa miundombinu ya majengo na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Utumishi wa Mahakama lililofanyika tarehe 9 Aprili, 2026 jijini Dodoma, Prof. Ole Gabriel ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo alisema Serikali imewekeza kwenye ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama kwa kutumia kiasi cha shilingi bilioni 144.
”Msisahau kwamba vipo Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki tisa (9) vinavyoendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini na vingine vinaelekea kukamilika vyenye thamani ya shilingi bilioni 74.6 na pia Serikali imewekeza kwenye mfumo wa kuwa na chumba maalum cha mifumo ya TEHAMA (Judiciary Situtional Room) ambacho kwa ubora ni cha pili duniani na cha kwanza Afrika”, alisema.
Alisema Serikali kuzindua minara 758 ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano pamoja na kuzindua uunganishi wa mifumo ya Mkongo huo kwenye wilaya takriban 85 kuna manufaa makubwa kwa Mahakama ya Tanzania kwa kuwa wilaya 85 zilizounganishwa zina majengo ya Mahakama hivyo mifumo hiyo iliyoboreshwa itasaidia kuimarisha utendaji kazi wa Mahakama.
Aidha, kwa upande wa Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Katibu wa Tume hiyo amesisitiza mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa na Watumishi hao ikiwemo kufanya kazi kwa bidii na kutobaguana na kuzingatia matumizi sahihi ya fedha za Umma ambapo aliwataka kutumia fedha hizo kwa kufuata taratibu zake.
Prof. Ole Gabriel pia alitoa wito kwa Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kuwa wabunifu katika kuendeleza matumizi ya TEHAMA na kwenda mbali zaidi kwenye matumizi hayo. Aliongeza kuwa Watumishi pia hawana budi kujiendeleza zaidi kielimu katika fani mbalimbali.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka ofisi za TUGHE Taifa Bw. James Limbu alimpongeza Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kusimamia vizuri suala la maslahi ya Watumishi.
Aidha aliwaasa watumishi kufanya kazi kwa bidii, maadili na weledi pasipo kumuangusha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
”Napongeza sana jinsi mnavyotekeleza mambo yenu hasa kusimamia na kutimiza maslahi ya Wafanyakazi”, alisema Mwakilishi huyo wa TUGHE Taifa.

