Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma Amuapisha Katibu Mpya wa Tume ya Utumishi wa Mahakama


Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemuapisha rasmi Prof. Elisante Ole Gabriel kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kufuatia kustaafu kwa aliyekuwa Katibu wa Tume hiyo, Bw. Mathias Kabunduguru.

Hafla hiyo fupi ya uapisho wa Katibu wa Tume imefanyika tarehe 10Septemba, 2021 katika Ofisi ndogo za Bunge zilizopo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kumuapisha Katibu wa Tume, Mwenyekiti wa Tume alimpongeza Prof. Elisante Ole Gabriel kwa kuaminiwa,kuteuliwa na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama.

Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama namba nne (4) ya mwaka 2011 kifungu cha 16 (ii) kinamtaka Jaji Mkuu wa Tanzania ambaye ndiye Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, kumuapisha Mtendaji Mkuu wa Mahakama kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.

“Mimi kama Mwenyekiti wa Tume tunakuahidi kukupa ushirikiano wakati wote ili kufanya majukumu yako kuwa mepesi, Binafsi nikakufahamu unapenda TEHAMA, hivyo ningependa kuona Tume ya Utumishi wa Mahakama ikitumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kutekeleza majukumu”. Alisema Mhe Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Naye,Katibu Mpya wa Tume Prof. Elisante Ole Gabriel alimuhakikishia Jaji Mkuu pamoja na Wajumbe wote wa Tume ya Utumishi wa Mahakamakuwa atafanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano kuhakikishamalengo yaliyokusudiwa na Tume yanafikiwa.

“Naomba niwahakikishie kuwa nitatumia uwezo wangu wote kuisimamia Tume katika suala la mchakato wa ajira, nidhamu na maadili ya Watumishi wa mahakama ili kufikia matarajio ya Tume,” Alisisitiza Prof.Elisante Ole Gabriel.

Hafla hiyo iliudhuriwa na Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Katibu Mstaafu Bw Mathias Kabunduguru, Naibu Katibu wa Tume Bi Enziel William Mtei pamoja na Watumishi wa Tume.