HAKI KATIKA MAJENGO MAPYA ILENGE KUMRIDHISHA MWANANCHI: JAJI MKUU
Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Busega
Jaji Mkuu na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa watumishi wa Mahakama na wadau wote katika mnyororo wa utoaji haki kuhakikisha kuwa haki inayotolewa katika majengo mapya ya Mahakama inalenga kumridhisha mwananchi.
Akizungumza baada ya kuzindua majengo 18 ya Mahakama za wilaya kwa wakati mmoja katika jengo jipya la Mahakama ya wilaya ya Busega, Jaji Mkuu pia aliwasihi wadau hao wa utoaji haki kutochafua taswira ya Mhimili huo wanapoyatumia majengo hayo mapya.
“Hakikisheni kuwa majengo haya hayageuzwi kuwa maeneo ambayo haki inachafuliwa na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa maadili. Mahakama ya Tanzania inapozungumzia uboreshaji wa huduma zake, ni pamoja na kuziba, maeneo yenye mianya na viashiria vya vitendo vya rushwa na utovu wa maadili”, alisema Mwenyekiti huyo wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Aliwataka wananchi kutoa taarifa kuhusu ukiukwaji wa maadili kwa kuwa taarifa hizo zitasaidia Uongozi wa Mahakama na taasisi nyingine za Umma zinazopambana na vitendo vya rushwa na utovu wa maadili kuwachukulia hatua watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Uzinduzi wa Mahakama ya Busega umewakilisha Mahakama nyingine 17 zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia katika wilaya za Busega, Itilima, Butiama, Rorya, Songwe, Gairo, Mkinga, Mbogwe, Nyang’hwale, Kyerwa, Missenyi, Kaliua, Uvinza, Buhigwe, Kakonko, Tanganyika, Kilombero na Mvomero.
Kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHEMA), Jaji Mkuu alisema majengo yote mapya ya Mahakama na yale ya zamani, yameunganishwa na mifumo ya TEHAMA hivyo Wananchi wanaopata huduma katika majengo haya watapata huduma inayoendana na mahitaji ya Karne ya 21.
Alisema baadhi ya faida watakazozipata wananchi kwa Mahakama kutumia TEHAMA kwenye majengo hayo 18 ya Mahakama za Wilaya ni pamoja na kutolewa kwa huduma inayozingatia Uwazi na Uwajibikaji (Transparency and Accountability) katika mtiririko wa utoaji wa uamuzi kwa kuwa taarifa zitapatikana kwa urahisi na haraka zaidi.
Jaji Mkuu alisema TEHAMA itasaidia viongozi wa Mahakama katika ngazi zote za Mahakama kushughulikia malalamiko kwa kuwa wana uwezo wa kuona kinachoendelea na kuboresha shughuli za Usimamizi wa Mashauri na Utawala.
Aidha, Kiongozi huyo wa Mhimili wa Mahakama aliishukuru Serikali kwa mchango wake mkubwa wa kutambua changamoto ya ukosefu na uchakavu wa miundombinu katika ngazi mbalimbali kote nchini na kuweka mipango ya ujenzi na ukarabati katika Mpango wa Serikali wa Maendeleo wa Miaka mitano mitano.
Akiwasilisha salamu za Mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Mkoa, Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda aliwakumbusha Maafisa wa Mahakama watakaohudumu katika Mahakama hizo za Wilaya kuzingatia Kanuni za Maadili ya Maafisa wa Mahakama kwa kutekeleza wajibu wao bila kujali hali ya kijamii au kiuchumi ya mhusika, na kutokuchelewesha haki bila sababu za msingi,
Mkuu huyo wa Mkoa alitoa wito kwa wadau mbalimbali wa Mahakama, wakiwemo Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea, Jeshi la Magereza na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama ili mashauri yaweze kumalizika kwa wakati.
“Niwaombe wananchi kutumia huduma za Mahakama mnapokuwa na migogoro badala ya kuchukua sheria mkononi, na mtakapokuwa na malalamiko kuhusu Mahakimu muwasilishe katika Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya Mkoa na Wilaya,” alisema. Mhe. Dkt. Nawanda.