RAIS SAMIA AIPONGEZA MAHAKAMA KWA KUIMARISHA SHUGHULI ZA UTOAJI HAKI
Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa hatua mbalimbali iliyochukua ili kuimarisha utoaji haki ikiwemo ugatuzi wa shughuli za Mahakama ya Rufani kwa kuanzia na Kanda tano za Mahakama Kuu.
Akitoa pongezi hizo kwa niaba ya Rais Samia leo tarehe 02 Februari, 2026 katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi alisema Rais Samia anaipongeza Mahakama kwa kuweza kugatua shughuli hizo katika mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Arusha. Mbeya na Tabora.
Makamu wa Rais alisema kuwa Rais Samia anatambua jitihada kubwa zinazofanywa na Mahakama katika kuimarisha utoaji haki nchini kwa kutunga Kanuni mbalimbali zilizosaidia kupunguza muda wa kusikiliza mashauri ya madai na jinai hadi kufikia miezi sita. Aidha, Kanuni 11 imetungwa ili kuboresha upatikanaji wa haki nchini.
Katika Hotuba yake iliyosomwa na Dkt. Nchimbi, Rais Samia ameshauri jitihada za Mahakama kwenda sambamba na usimamizi wa dhamana kwa watuhumiwa wenye stahiki za kisheria kupata haki mahakamani. Hatua hii itawawezesha watuhumiwa kuendelea na shughuli za maendeleo wakiwa kwenye dhamana.
‘Natoa rai kwa wadau wote wa Mahakama kuunga mkono jitihada hizi kwa ustawi na maendeleo ya Taifa letu kwa kuzingatia kuwa zoezi hilo la dhamana linahusisha pia Taasisi nyingine”, ilisema sehemu ya hotuba hiyo.
Kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Rais Samia pia ameipongeza Mahakama kwa kuanza ujenzi wa mfumo wa Akili Unde kwa ajili ya kuchukua mwenendo na kumbukumbu za mashauri mahakamani. Alisema kuwa hatua hii itasaidia kuleta ufanisi katika utoaji wa haki.
Akizungumzia Kauli mbiu ya maadhimisho hayo inayosema, ‘Mchango wa Mahakama katika Ustawi na Maendeleo ya Taifa,’ Rais Samia ameeleza kuwa imebeba ujumbe muhimu unaonesha kuwa Mahakama si tu Mhimili uliojikita katika kutoa haki pekee, bali ni nguzo muhimu ya ustawi wa jamii, maendeleo ya kiuchumi na ustawishaji wa amani ya Taifa.
‘Mahakama ndiyo Mhimili ambao unahakikisha kuwa haki inapatikana kwa wote bila upendeleo wala uonevu wa aina yoyote. Mahakama siyo tu chombo cha mwisho cha utoaji haki nchini, bali ni mshirika muhimu katika safari ya maendeleo ya Taifa,’ alisema.
Alisema kutokana na umuhimu wa Mahakama katika ujenzi wa Taifa, Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi katika kuimarisha uhuru wa Mahakama ili kuiwezesha kutekeleza wajibu wake kikamilifu na kuchochea ustawi na maendeleo ya Taifa. Lengo la hatua hizi ni kutekeleza dhamira ya Serikali ya kujenga Taifa lenye amani na uchumi jumuishi na imara.
Alisema Serikali itaendeleza ushirikiano wake na Mahakama katika ujenzi wa miundombinu ya Mahakama, kuimarisha rasimilimaliwatu na kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama na kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi, hususan kupitia mpango wa ujenzi wa Mahakama za Mwanzo.
Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini kwa mwaka 2026, yamefanyika kitaifa leo katika Viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na Mahakama ya Tanzania.

