IJUE TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA NA JUKUMU LAKE LA USIMAMIZI WA MAADILI


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Moja ya jukumu la Tume ya Utumishi wa Mahakama ni kusimamia Maadili ya Maafisa wa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi. Jukumu la kusimamia maadili ya Maafisa wa Mahakama pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu na. 29 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Namba 4 ya mwaka 2011. Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Bi. Enziel Mtei alifanya mahojiano maalumu na Mwandishi wetu Lydia Churi kuhusu Tume ya Utumishi wa Mahakama na Jukumu lake la kusimamia Maadili ya Maafisa wa Mahakama. Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo……………….

Swali: Tume ya Utumishi wa Mahakama ni nini, inaundwa na akina nani na wajumbe wake wanapatikanaje?

Jibu: Kwa mujibu wa Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Utumishi wa Mahakama inaundwa na wajumbe wafuatao; Jaji Mkuu ambaye ni Mwenyekiti, Mwanasheria Mkuu wa Serikjali ni mjumbe, Jaji mmoja wa Mahakama ya Rufani ambaye anateuliwa kwa ajili jhiyo na Rais baada ya kushauriwa na Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye ni mjumbe pamoja na wajume wawili wanaoteuliwa kwa mujibu wa kifungu cha 15 (1) cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Namba 4 ya mwaka 2011. Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ni Katibu wa Tume na ndiye mtekelezaji wa maamuzi yote ya Tume. Aidha, ipo Sekretarieti inayosaidia Tume kwenye utekelezaji wa majukumu yake.

Swali: Ni nini majkukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa mujibu wa Sheria?

Majukumu ya Tume yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhurti ya Muungano wa Tanzania na kifungu Na. 29 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Namnbba. 4 ya mwaka 2011 kama ifuatavyo; Kumshauri Rais kuhusu;

-Uteuzi wa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Msajili Mkuu, Msajili wa Mahakama ya Rufani na Msajili wa Mahakama Kuu.

-Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi au Jaji wa Mahakama Kuu anaposhindwa kutekeleza majukumu yake

-Mwenendo wa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi na Jaji WA Mahakama Kuu pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Msajili Mkuu, Msajili wa Mahakama Kuu ambao hauendani na maadili ya kazi yake au sharia zinazosimamia maadili ya viongozi wa Umma.

-Mishahara na maslahi ya watumishi wa Mahakama

-Kufanyia uchunguzi malalamiko dhidi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi au Jaji wa Mahakama Kuu

-Kufanya uteuzi, kuthibitisha, kupandisha cheo na kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wasio Maafisa wa Mahakama.

-Kuajiri, kupandisha cheo na kuchukua hatua zozote za kinidhamu dhidi ya watumishi wasio Mahakimu. Tume pia imepewa mamlaka na sheria ya kuteua viongozi mbalimbali wa Mahakama wakiwemo Naiubu Wasajili na Watendaji wa Mahakama.

Swali: Umetaja kuwa, mojawapo ya majukumu ya Tume ni kusimamia maadili ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania. Je upo mfumo au Kamati zozote zilizoundwa kuisaidia Tume kwenye jukumu hili?

Jibu: Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Namba 4 ya mwaka 2011 kimeiruhusu Tume ya Utumishi wa Mahakama kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni; Kamati ya Maadili ya Majaji, Kamati ya maadili ya Maafisa wa Mahakama, Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama ya Mkoa na Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama ya wilaya.

Swali: Unaweza kuwafahamisha wananchi kwamba kamati za Maadili hususan za mikoa na wilaya zinaundwa na akina nani?

Jibu: Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama ya Mkoa inaundwa na wajumbe wafuatao; Mkuu wa Mkoa ndiye, wajumbe ambao ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa, wajumbe wawili wanaoteuliwa na Mkuu wa Mkoa, Maafisa wawili wa Mahakama wanaoteuliwa na Jaji Mfawidhi. Katibu wa kamati hiyo atakuwa ni Mwanasheria wa Serikali Mfawidhi, katika mkoa wenye ofisi ya Mwanansheria Mkuu wa Serikali.  

Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya wilaya inaundwa na wajumbe ambao ni Mkuu wa wilaya (Mwenyekiti), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya, Katibu Tawala wa wilaya (Katibu) wajumbe wawili watakaoteuliwa na Mkuu wa wilaya pamoja na Mahakimu wawili watakaoteuliwa na Jaji Mfawidhi.

Swali: Je majukumu ya Kamati za Maadili ni yapi?

Jibu: Kupokea malalamiko yanayohusu Afisa wa Mahakama yanayohusu Mahakimu, kufanyia uchunguzi malalamiko/tuhuma, kumuonya Afisa wa Mahakama juu ya malalamiko dhidi yake kama suala hili halihitaji kupelekwa mbele ya Tume na kuchukua hatua itakayofaa kulingana na mazingira ama aina ya malalamiko.

Swali: Unawezaje kutofautisha majukumu ya Kamati ya maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya mkoa na ya wilaya?

Jibu: Majukumu ya kamati za maadili ya Maafisa wa Mahakama ya Mikoa na wilaya yanafanana na tofauti iliyopo ni kwamba kamati ya Mkoa inashughulikia Mahakimu Wakazi ngazi ya Mkoa na Wilaya na kamati ya wilaya inashughulikia Mahakimu wote walioko kwenye Mahakama za Mwanzo nchini.

Swali: Umeeleza kuwa kamati zinapokea na kuchunguza malalamiko. Je ni nani anaweza kuwasilisha malalamiko kwenye kamati?

Jibu: Mtu au Taasisi yoyote inaweza kuwasilisha malalamiko yake mbele ya Tume au Kamati zake iwapo kutakuwepo na ushahidi. Mfano wa; Afisa Mahakama, Afisa Sheria, Wakili wa Serikali, Wakili wa kujitegemea, Taasisi ya Serikali na mtu yeyote mwenye ushahidi wa kutosha juu ya malalamiko yake.

Swali: Je upo utaratibu wowote uliowekwa na sheria wa namna ya kuwasilisha malalamiko?

Jibu:  Malalamiko yote yanapaswa kuwasilishwa kwa maandishi na yawe na sahihi ya mlalamikaji. Aidha, malalamiko hayo yanapaswa kuwa na taarifa za kutosha kama vile maelezo ya kitendo kilichotendeka na mazingira yake, mfano ni namna shauri lilivyoshughulikiwa, tuhuma za rushwa, kushindwa kutekeleza majukumu na vitengo vinavyokiuka kanuni za maadili ya Maafisa wa Mahakama.

Swali: Kutokana na umuhimu ulioueleza wa majukumu ya kamati za maadili katika kusimamia maadili ya Maafisa wa Mahakama, Je Tume inafanya nini kuhakikisha kuwa kamati zinatekeleza iupasavyo majukumu yake?

Jibu: Tume imekuwa ikitoa mafunzo kwa wajumbe wa kamati za Maadili, Tume pia imeandaa mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kuona namna Kamati zinavyofanya kazi pamoja na kutoa elimu ya kurekebisha kasoro zinazoonekana na kufanya ziara ambapo hukutana na wajumbe wa kamati za maadili kwa lengo la kuwapa elimu pamoja na kuwakutanisha ili wapate nafasi ya kubailishana uzoefu. 

Swali: Pamoja na Tume kuwa ni Mamlaka ya nidhamu, Mahakama inalalamikiwa kwa ukiukwaji wa maadili hususan kwa Mahakimu ambao ndiuyo wamepewa jukumu la kutoa haki. Unazungumziaje hili?

Jibu: Mahakama kama zilivyo taasisi nyingine za Umma, baadhi ya watumishi wake wanalalamikiwa kukiuka maadili ya utendaji wao ikiwemo vitendo vya rushwa. Baadhi ya watumishi pia wanatuhumiwa kwa utoro, kutoa siri za ofisi, kughushi nyaraka, uzembe, ulevi uliuopindukia, kuvaa mavazi yasiyo na heshima, wizi n.k vitendo hivi vinaathiri utoaji haki na kuharibu taswira ya Mahakama. Tume unaendelea kuelekeza wasimamizi wote wa kazi kuwaelimisha watumishi walio chini yao kuhusu kufuata maadili pamoja na athari wanazoweza kuzipata iwapo watabainika kutozingatia maadili.

Tume inaendelea na utaratibu wa kufanya ziara kwenye mikoa yote kuzungumza na watumishi na kusisistiza suala la maadili. Aidha Tume inaendelea kuzijengea uwezo kamati za maadili ili kuziwezesha kutekeleza majukumu yake kwa kufuata misingi ya Sheria, kanuni na taratibu.

-Mahakama pia imeongeza uwazi kupitia matumizi ya mifumo ya TEHAMA kuhusu taratibu za upatikanaji wa huduma mahakamani pamoja na namna ya kuwasilisha malalamiko yoyote kuhusu kutoridhishwa na huduma, ukiukaji wa maadili au maoni yenye lengo la kusaidia kuboresha huduma.   

-Tume inachukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wanaobainika kukiuka maadili. Kutokana na kuchukuliwa kwa hatua hizo, utafiti wa hivi karibuni unaonesha kuimarika kwa maadili hasa kupungua kwa vitendo vya rushwa, mfano mwaka 2018 jumla ya Maafisa 27 wa Mahakama waliokuwa wamefikishwa mahakamani kwa ukiukwaji wa maadili, 24 yalihusu rushwa. Kutokana na hatua zinazochukuliwa na Tume pamoja na Uongozi wa Mahakama, kwa sasa kumbukumbu zinaonesha kuwepo kwa Afisa Moja mwenye tuhuma mahakamani. Haya ni mafanikio na kwa upande mwingine Imani ya wananchi na wadau kwa Mhimili wa Mahakama inazidi kuongezeka.

Swali: Katika kutekeleza majukumu yake, Tume ya Utumishi wa Mahakama inakabiliwa na changamoto zipi?

Jibu: Changamoto tuliyonayo sasa kwenye suala la usimamizi wa Maadili kupitia kamati za Maadili ni kwamba wananchi walio wengi hawana uelewa wa kuwepo kwa kamati za Maadili.

-Inawezekana kuwa kitendo cha wananchi kutofahamu kuhusu uwepo wa kamati hizi hata kama vipo vitendo vya ukiukwaji wa maadili havitolewi taarifa.

-Vitendo vya ukiukwaji wa maadili vikiachwa viendelee vitachafua taswira ya Mhimili wa Mahakama lakini pia baadhi ya wananchi wanaweza kuchelewa kupata haki zao zilizowekwa na sheria au hata kuzikosa kabisa.

Swali: Je Tume ya Utumishi wa Mahakama inaishughulikiaje Changamoto uliyoieleza?

Jibu:  Mojawapo ya malengo ya ziara zinazofanywa na Tume kwenye mikoa mbalimbali ni kutoa elimu kwa Umma kwa kuwa wakati wa ziara hizo Tume huwaalika pia Wanahabari ambao nao husaidia kuwaelimisha zaidi wananchi.

  • Kuwahusisha viongozi wa mikoa na wilaya kwenye suala la kutoa elimu wanapokuwa na mikutano ya hadhara kwenye maeneo yao.
  • Kuandaa machapisho mbalimbali yanayoelezea Tume pamoja na kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama.
  • Kushiriki kwenye Maonesho mbalimbali ya kitaifa na kikanda kwa lengo la kutoa elimu.
  • Kutoa elimu kwa njia Televisheni na Redio