WAJUMBE KAMATI ZA MAADILI MKOA WA DODOMA WAAPISHWA
- Awataka kutenda Haki na Kutunza Siri
Na Arapha Rusheke, Mahakama Kuu Dodoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt Juliana Masabo amewaapisha baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa na ngazi ya Wilaya na kuwataka wajumbe hao kutekeleza majukumu yao kwa kutenda haki.
Akizungumza mara baada ya kuwaapisha wajumbe hao tarehe 9, Juni, 2025 katika ukumbi wa Mikutano uliopo Kituo jumuishi cha utoaji haki (IJC) Dodoma, Jaji Mfawidhi pia aliwataka wajumbe wote wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa na Wilaya kutekeleza jukumu lao la msingi la kusimamia maadili ya Mahakimu kwa uaminifu na kwa weledi.
”Tendeni haki mnapotekeleza jukumu lenu la msingi la usimamizi wa maadili na nidhamu ya Mahakimu, muwe na utamaduni wa kutoa nafasi ya kuwasikiliza wale wanaofikishwa mbele ya Kamati zenu ili muweze kutenda haki”, alisema Mhe. Dkt Masabo.
Akizungumzia umuhimu wa mafunzo kwa wajumbe wa Kamati za Maadili yanayoratibiwa na Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dkt Masabo alisema yana umuhimu mkubwa kwa kuwa yatawajengea uwezo na kuwaimarisha wajumbe katika utekelezaji wa majukumu yao.
Jaji huyo aliwakumbuka wajumbe umuhimu wa kutunza siri za kamati na kufanya uamuzi wa pamoja wanapokuwa katika vikao vya kamati. Aliongeza kuwa wajumbe hao hawana budi kuwa kioo cha wengine kwa kuwa na maadili na nidhamu.
Vilevile Dkt Masabo alitumia wasaa huo kwa kuwapatia elimu kuhusu kanuni za uendeshaji wa kamati za maadili ya Maafisa Mahakama ambazo zitawasaidia katika utendaji kazi wao. Aidha, baada ya kupatiwa mafunzo, wajumbe walionesha kufurahia kitendo hicho cha kuelimishwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama mkoani humo Mhe. Rosemary Senyamule amewasisitiza wajumbe wa Kamati ya Mkoa kukutana na kufanya vikao vya kamati na kuhakikisha vikao hivyo vinafanyika kwa wakati kwa mujibu wa Sheria. Lakini pia ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa maboresho mazuri ambayo yanaendelea kuonekana kwa Wananchi kwa Ujumla.
Mhe. Senyamule aliwataka wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa kutekeleza wajibu wake wa kusimamia maadili na nidhamu ya Mahakimu kwa kufuata taratibu na Sheria zilizowekwa.
Walioapishwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule (Mwenyekiti), Wakuu wa wilaya za Dodoma, Chamwino Ikulu, Kongwa, Mpwapwa, Bahi, Chemba na Kondoa (Wenyeviti) pamoja na wajumbe wengine wa Kamati ngazi ya Mkoa na wilaya za Mkoa wa Dodoma.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.
Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia kwenye jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.
(Habari hii imehaririwa na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama)