TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA YAMUAGA JAJI NDIKA
Na Selina Mlelwa, Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Tume ya Utumishi wa Mahakama imemuaga rasmi aliyekuwa Mjumbe wa Tume, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Gerald Ndika baada ya kumaliza muda wa kuwa Mjumbe wa Tume hiyo kwa mujibu wa Sheria.
Hafla ya kumuaga Jaji Ndika imefanyika tarehe Mei 15, 2026 katika ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama jijini Dodoma wakati wa kikao cha Tume kinachokutana kwa mujibu wa Sheria.
Jaji Dkt. Ndika amekuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa vipindi viwili vya miaka mitatu sawa na miaka sita kwa mujibu wa sheria.
Hafla hiyo ya kumuaga Jaji Ndika iliongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. George Masaju ambapo wajumbe wa Tume na viongozi wengine walipata fursa ya kutoa shukrani na pongezi kwa mchango mkubwa alioutoa katika kuimarisha utendaji kazi wa Tume kwa kipindi chote alichohudumu kama Mjumbe wa Tume.
Awali akizungumza, Jaji Dkt. Ndika alishukuru kipekee kwa ushirikiano aliopewa na Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi, Wajumbe wa Tume, viongozi wengine pamoja na Sekretarieti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Aidha, Mhe. Dkt. Ndika aliitaka Sekretarieti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia utunzaji wa siri, weledi pamoja na kufuata tamaduni na maadili ya kazi za Tume ili kuendelea kudumisha ufanisi na heshima ya Taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu alimpongeza Mhe. Dkt. Ndika kwa unyenyekevu wake na kusema kuwa hashangazwi na uteuzi wake kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya kutathmini masuala ya ardhi katika Wilaya ya Ngorongoro kutokana na uwezo wake mkubwa wa uongozi na utendaji kazi.
Sambamba na hayo, Mhe. Masaju alisisitiza umuhimu wa Sekretarieti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kuzingatia siri za kazi, maadili pamoja na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili kuendelea kulinda hadhi na ufanisi wa Taasisi.
Mhe. Dkt. Gerald Ndika ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na ameitumikia Tume ya Utumishi wa Mahakama KAMA Mjumbe wa Tume kwa awamu mbili, sawa na miaka sita, kwa mujibu wa sheria.

