SHUGHULIKIENI MASHAURI YA KINIDHAMU KWA WAKATI NA KWA USAHIHI: PROF. OLE GABRIEL
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka Wajumbe wa Kamati za Nidhamu za Watumishi wasio Maafisa Mahakama kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu zilizowekwa wanaposhughulikia mashauri ya kinidhamu ili kutenda haki kwa watumishi wote.
Akifunga mafunzo ya siku mbili ya Wajumbe wa Kamati za Nidhamu za Watumishi wasio Maafisa Mahakama tarehe 5 Juni, 2026 jijini Mwanza Mtendaji Mkuu wa Mahakama amesema mashauri hayo ya kinidhamu yasiposhughulikiwa kwa wakati na kwa usahihi husababisha malalamiko kutoka kwa watumishi na hivyo kuweza kuathiri utendaji kazi wa taasisi.
Aidha, amewataka wajumbe wa Kamati hizo kuepuka kufanya kazi kwa mazoea kwani kwa kufanya hivyo watadhoofisha jukumu la msingi la Mahakama la kusimamia haki, uwajibikaji na utawala bora katika maeneo yao ya kazi.
Katibu huyo wa Tume ya Utumishi wa Mahakama pia amewataka wajumbe wa Kamati za Nidhamu za watumishi wasio Maafisa Mahakama kuzingatia usiri wa taarifa za watumishi wanapotekeleza majukumu yao ili kulinda haki za watumishi wanaofikishwa kwenye kamati hizo.
Kuhusu ushirikiano, Prof. Ole Gabriel ametoa wito kwa Watumishi wa Mahakama kuendeleza ushirikiano na kudumisha umoja hususan wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku ya kutoa haki huku akibainisha kuwa watumishi wasio Maafisa Mahakama wana mchango mkubwa katika mnyororo wa utoaji haki.
Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama iliandaa Mafunzo ya siku mbili kwa wajumbe wa Kamati za Nidhamu za Watumishi wasio Maafisa Mahakama yaliyolenga kuwajengea uwezo wajumbe hao wanapotekeleza majukumu yao na kuimarisha kamati hizo.

