JAJI MFAWIDHI MWANZA ATOA WITO KAMATI ZA NIDHAMU KUZINGATIA SHERIA


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga ametoa wito kwa Wajumbe wa Kamati za Nidhamu za Watumishi wasio Maafisa Mahakama kutekeleza majukumu yake kwa haki, uwazi, kufuata taratibu za kisheria na pasipo kukiuka haki za Mtumishi.

Akifungua mafunzo ya siku mbili ya Wajumbe wa Kamati za Nidhamu za Watumishi wasio Maafisa Mahakama tarehe 4 Juni, 2026 jijini Mwanza, Jaji Mfawidhi alisema elimu inayotolewa na Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa Kamati hizo itazisaidia kutekeleza majukumu yake kwa haki pia itapunguza malalamiko ya kutotendewa haki na rufaa zisizo za lazima.

Alitoa rai kwa wajumbe hao kusikiliza kwa makini mada zitakazowasilishwa kwa lengo la kuleta ufanisi na kuwapatia watumishi wasio Maafisa Mahakama kile kinachokusudiwa.

Alisema kupitia mafunzo hayo, wajumbe wa kamati hizo pia watapata  fursa nzuri ya kujadiliana na kubadilishana uzoefu kuhusu njia bora za kushughulikia mashauri ya kinidhamu ya watumishi wasio Maafisa Mahakama.

Akizungumzia nidhamu kwa watumishi wa Mahakama Mhe. Kilekamajenga alisema kuwa Mahakama ni taasisi inayohitaji watumishi wake kuwa na nidhamu na maadili ya hali ya juu kwa kuwa jukumu lake la msingi ni kutoa haki kwa wananchi.

”Ukiikuta Taasisi ina nidhamu ya hali ya juu ujue kuwa taasisi hiyo ina  taratibu imara za kuchukuliana hatua”, alisema.

Alisema kutokana na majukumu ya Mahakama, Wajumbe wa Kamati za Nidhamu wanapaswa kuwa wakali zaidi kwa Watumishi wanaokiuka taratibu za kazi kwa kuwa vitendo hivyo havimchafui Mtumishi husika  peke yake bali vinachafua taasisi nzima.

”Watumishi wavivu, wazembe na watoro kazini hawana budi kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu kwa kuwa Mahakama inatazamwa kwa ujumla wake, Mtumishi moja wa Mahakama akikosea basi inatazamwa Mahakama nzima”, alisisitiza.

Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Maadili na Nidhamu) Bi. Alesia Mbuya alisema kupitia mafunzo hayo, Tume inatarajia kuwajengea uwezo wa pamoja wajumbe wa Kamati za Nidhamu katika uanzishaji, uchambuzi,ushughulikiaji, uhitimishaji wa mashauri ya nidhamu, utunzaji wa kumbukumbu, uandishi wa taarifa na utekelezaji wa maamuzi ya kamati kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Naibu Katibu alisema kuwa mafunzo kwa Kamati hizo ni moja ya utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama na msingi wa utawala bora unaozingatia sheria, kanuni na taratibu pamoja na miongozo katika usimamizi wa utekelezaji wa majukumu ya Tume.