JAJI KARAYEMAHA AWAAPISHA WAJUMBE WA KAMATI ZA MAADILI MKOANI RUVUMA


  • Awataka kutenda Haki na Kutunza Siri

Na Lydia Churi- Tume ya Tumishi wa Mahakama, Songea 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea Mhe. James Karayemaha amewaapisha baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa na ngazi ya Wilaya na kuwataka wajumbe hao kutekeleza majukumu yao kwa kutenda haki.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha wajumbe hao jana mjini Songea, Jaji Mfawidhi pia aliwataka wajumbe wote wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa na Wilaya kutekeleza jukumu lao la msingi la kusimamia maadili ya Mahakimu kwa uaminifu na kwa weledi.

”Tendeni haki mnapotekeleza jukumu lenu la msingi la usimamizi wa maadili na nidhamu ya Mahakimu, muwe na utamaduni wa kutoa nafasi ya kuwasikiliza wale wanaofikishwa mbele ya Kamati zenu ili muweze kutenda haki”, alisema Mhe. Karayemaha.

Wajumbe walioapishwa ni Mkuu wa Wilaya ya Songea Bw. Kapenjama Ndile ambaye anakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama wilaya ya Songea na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea Mhe. Asha Hassan Waziri ambaye anakuwa ni Mjumbe wa Kamati ya Maadili ya Mkoa wa Ruvuma. Aidha, Mwalimu Mstaafu mama Ngwala pia aliapishwa kuwa Mjumbe wa Kamati hiyo.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo kwa wajumbe wa Kamati za Maadili yanayoratibiwa na Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama, Jaji Karayemaha alisema yana umuhimu mkubwa kwa kuwa yatawajengea uwezo na kuwaimarisha wajumbe katika utekelezaji wa majukumu yao.

Jaji huyo aliwakumbuka wajumbe umuhimu wa kutunza siri za kamati na kufanya uamuzi wa pamoja wanapokuwa katika vikao vya kamati. Aliongeza kuwa wajumbe hao hawana budi kuwa kioo cha wengine kwa kuwa na maadili na nidhamu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama mkoani humo Col. Ahmed Abbas Ahmed amewasisitiza wajumbe wa Kamati ya Mkoa kukutana na kufanya vikao vya kamati na kuhakikisha vikao hivyo vinafanyika kwa wakati kwa mujibu wa Sheria.

Aidha aliwataka wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa kutekeleza wajibu wake wa kusimamia maadili na nidhamu ya Mahakimu kwa kufuata taratibu na Sheria zilizowekwa.

Kuhusu kuwezesha kufanyika kwa vikao vya Kamati, Mkuu huyo wa Mkoa aliagiza kutengwa kwa bajeti ya kuwezesha vikao hivyo.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi. 

Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237. 

Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia kwenye jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye Kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.