JAJI MKUU AMUAPISHA DKT. JINGU KUWA KATIBU MPYA WA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. George Masaju amemuapisha Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Dkt. John Jingu kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Hafla ya Uapisho wa Dkt. Jingu imefanyika leo tarehe 26 Juni, 2026 katika Ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na watumishi wa Sekretariet ya Tume.
Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alimteua Dkt. Jingu kuchukua nafasi ya Prof. Elisante Ole Gabriel ambaye amestaafu Utumishi wa Umma kwa mujibu wa Sheria.
Kwa mujibu wa kifungu cha 15 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ndiye Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Mtekelezaji wa maamuzi ya Tume.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kwa lengo la kusimamia Utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania.
Tume ndiyo inayosimamia ajira na nidhamu ya watumishi wote wa Mahakama. Mamlaka haya ya Tume kama Msimamizi wa ajira na nidhamu za watumishi wa Mahakama yanatokana na Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa Pamoja na kifungu cha 29 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.

