JAJI MKUU AWATAKA MANAIBU WASAJILI KUZINGATIA MASLAHI YA UMMA NA YA TAIFA


  • Jaji Kiongozi Awaapisha Manaibu Wasajili 31

Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. George Masaju amewataka Manaibu Wasajili kuzingatia maslahi ya Umma na ya Taifa wanapotekeleza majukumu yao ili kulinda, kutunza na kuheshimu mamlaka na uhuru wa Mahakama. 

Jaji Mkuu wa Tanzania ameyasema hayo jana tarehe 17 Juni, 2026 jijini Dodoma, alipokuwa akizungumza na Manaibu Wasajili 31wa Mahakama ya Tanzania walioapishwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Dkt. Mustapher Siyani katika ukumbi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama jijini Dodoma.  

Alisema kuwa Manaibu Wasajili ni kada muhimu na ni injini katika utendaji kazi wa kila siku katika ngazi zote za Mahakama hivyo amewataka Viongozi hao kujitambua na kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maslahi ya Umma na Taifa kwa ujumla.

“Tumetambua kuwa mnazo sifa za kuwa Viongozi na Tume imewateua, basi nendeni mkaziishi sifa hizo lakini pia tambueni kuwa tunaishi nyakati ambazo  uwajibikaji unasisitizwa, tusifurahie tu kuteuliwa, kila nafasi ya uongozi na ya mafanikio inakuja na wajibu mkubwa kwa mhusika”, alisema Jaji Mkuu.

Alisema ingawa Manaibu Wasajili watapatiwa mafunzo, ni matarajio yake kuwa tayari wana ufahamu wa majukumu yao kutokana na uzoefu walionao pamoja na baadhi yao kukaimu nafasi za Uongozi na wengine kuwa Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya. Aliongeza kuwa kwa nafasi ya Manaibu Wasajili mambo ni yale yale.

Aidha, amewataka Manaibu Wasajili hao kusoma Sheria zinazoelezea majukumu yao ili wawe na uelewa mpana na kuwa kwenye nafasi nzuri ya kutekeleza ipasavyo majukumu yao.” Jitambueni muwajibike kama viongozi katika maeneo yenu ya kazi, jitoleeni kwa moyo wote ili kuleta ufanisi”, alisema Jaji Mkuu.

Kuhusu mashauri mahakamani, Jaji Mkuu amewataka Manaibu Wasajili kudhibiti na kupunguza mlundikano wa mashauri katika masjala zao na kutoa kipaumbele kwa mashauri ya mirathi hususan yanayowahusisha makundi ya watu wenye uhitaji maalum katika jamii (vulnerable) na kuhakikisha wanamaliza mapema mashauri ya watu hao.

Jaji Mkuu pia amewataka Manaibu Wasajili kusimamia ipasavyo utekelezaji wa hukumu kutokana na eneo hilo kuwa na changamoto ambapo aliwasisitiza kuwa makini na waadilifu katika utekelezaji wa hukumu.

Kuhusu utekelezaji ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Jaji Mkuu alisema Mahakama itaendelea kuwa na mchango mkubwa na wa kipekee katika utekelezaji wa Dira hiyo inayosisitiza Utawala Bora na Amani ya jamii.

Aidha, amewataka Manaibu Wasajili kutambua kuwa taifa haliwezi kuwa na maendeleo bila ya kuwa na amani hivyo wanapaswa kutenda kazi kwa kuzingatia utawala wa sheria kama ilivyoelekezwa katika Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.    

Uteuzi wa Manaibu Wasajili wa Mahakama ya Tanzania ni utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama. Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mahakama sura ya 237, vinaipa Tume jukumu la kuteua, kupandisha cheo na kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya Watumishi wote wa Mahakama isipokuwa wale ambao sio mamlaka ya uteuzi wa Tume.